Tamthilia ya Noma, Sultan Tamba zang’ara Tuzo za ZIFF 2026

ZANZIBAR:WASANII wa Tanzania, Uganda na Kenya wameibuka vinara katika Tuzo za Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) 2026 zilizohitimishwa usiku wa Juni 28, huku ushindi ukionesha ukuaji wa tasnia ya filamu Afrika na ushindani mkubwa kati ya kazi za kitaifa, Afrika Mashariki na bara zima.
Miongoni mwa matukio makubwa ya tamasha la mwaka huu ni kuanzishwa kwa kategoria mpya ya filamu zilizotengenezwa kwa kutumia Teknolojia ya Akili Bandia (AI Film), ambapo Mtanzania Sultan Tamba aliandika historia kwa kutwaa tuzo ya kwanza kupitia filamu yake Kilwa Kisiwani, hatua inayodhihirisha uwezo wa wabunifu wa ndani kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Katika ngazi ya Tanzania, tamthilia ya Noma ilitawala tuzo za mfululizo wa runinga baada ya kutwaa tuzo ya Tamthilia Bora chini ya waandaaji Khaleed Mfundo na Adam Kibaro. Aidha, Sadam Nawanda na Magdalena Munis walinyakua tuzo za Muigizaji Bora wa Kiume na Muigizaji Bora wa Kike, huku filamu ya Couple Goals ikiwapa Prince Jimmy na Chuchu Hansy tuzo za waigizaji bora katika filamu za Tanzania.
Kwa upande wa Afrika Mashariki, Uganda iliibuka mshindi mkubwa kupitia filamu Small Gods iliyoongozwa na Asher Rosen, iliyotwaa tuzo za Filamu Bora ya Afrika Mashariki pamoja na Muigizaji Bora wa Kiume na Muigizaji Bora wa Kike zilizokwenda kwa Turinayo Jonathan na Chimpanye Florence Mariserena. Filamu ya Lice N’ Shine nayo iliiongezea Uganda tuzo ya Filamu Bora ya Vibonzo.
Kenya nayo ilifanya vizuri katika kategoria za tamthilia za Afrika Mashariki, ambapo Kash Money Season 1 ilitwaa tuzo ya Tamthilia Bora, huku Sanaipei Tande na Mike Saruni wakishinda tuzo za waigizaji bora wa kike na wa kiume kupitia kazi zao katika tamthilia za Afrika Mashariki.
Katika ngazi ya Afrika, filamu A Land Apart kutoka Nigeria ilitangazwa kuwa Filamu Bora ya Mwaka 2026, wakati We Are Hadza kutoka Tanzania na Marekani ilitwaa Tuzo ya Mwenyekiti. Filamu Eyes of Ghana ilishinda tuzo nyingine muhimu, huku Elda kutoka Ethiopia, Prank (Jokes on You) kutoka Zambia na Amazeze (Flease) kutoka Afrika Kusini nazo zikitunukiwa tuzo katika kategoria mbalimbali.
Mbali na ushindi wa filamu, ZIFF 2026 pia ilitambua mchango wa wadau wa maendeleo ya sanaa, ambapo Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Grau, alitunukiwa Tuzo Maalum ya Balozi Mtetezi wa Sanaa. Matokeo ya mwaka huu yameonesha kuimarika kwa ubora wa filamu za Afrika na kufungua ukurasa mpya wa matumizi ya teknolojia ya Akili Bandia katika tasnia ya filamu.



