BurudaniFilamu

ZIFF yaweka wazi Tuzo ya Sembene Ousmane

TAMASHA la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) limesema litakuwa tena na shindano la Tuzo ya Filamu ya Sembene Ousmane mwaka 2023.

Tuzo hizo huzingatia filamu za kimaendeleo na kila tuzo mshindi huondoka na Euro 3,000 sawa na shilingi milioni 7.6 kila mmoja.

Sembene ni mtayarishaji sinema wa Senegal ambaye pia anachukuliwa kama Baba wa Sinema ya Afrika.

Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Profesa Martin Mhando amesema kwamba toka mwaka 2011 ilipoanzishwa tuzo ya Sembene, imetoa msukumo mkubwa katika nyanja za filamu fupi za kubuniwa na za makala.

Ametaja mfano wa filamu hizo kuwa kama vile Ramata- Toulaye SY, (Senegal), Samir Ahmed (Misri), Ekwa Msangi (Tanzania), Marie- Clementine Dusambejambo (Rwanda) na zote zimedhihirisha ubora wa tuzo.

“Mwaka huu tunatayarisha tena filamu 17 zitakazoshindana. Tanzania inaongoza
kwa kuwa na filamu 4 zinazowania tuzo hizo,” amesema Profesa Mhando.

Amesema filamu hizo ni pamoja na filamu ya Katope ambayo ni ya kutisha iliyowahi kushinda tuzo ya filamu bora katika Tuzo za Filamu Tanzania kwa mwaka 2021.

“Katope ni filamu mpya ambayo imeongozwa na Walt Mzengi, mshindi wa shindano kubwa la Netflix mwaka 2022. Hii ni filamu yenye viwango vya juu vya utayarishaji na ilipigwa picha Dodoma na inakuja wiki chache tu baada ya kuoneshwa kwa mara ya kwanza na
Netflix kimataifa,” anasema Profesa Mhando.

Mwana Hiti ya Nicholas Mwakatobe na Haikaeli Kinyamagoha, ndiyo filamu ya makala pekee katika orodha ya Tanzania.

Filamu ya mwisho ni Nia ya Azad Wastara, mtayarishaji mpya wa mitindo wa ubunifu wa
kisayansi.

Pamoja na Tanzania kuingiza sinema hizo inakabiliwa na changamoto kali kutoka kwa filamu kama ya Act of Love (Kenya), Neb Tawn (Misri) na In the Stillness (Nigeria).

“Tamasha pia limeamua kuzawadia sio moja tu, bali filamu tatu, ili kuhakikisha kuwa wasanii wengi wa filamu wanahamasishwa kutengeneza filamu za ubunifu kupitia Tuzo ya
Sembene Ousmane,” amesema Profesa Mhando.

Related Articles

Back to top button