Tamasha la TaSUBA kufanyika Oktoba 23 hadi 26

BAGAMOYO: MAANDALIZI ya Tamasha la 43 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linalotarajiwa kuanzia Oktoba 23 hadi 26 mwaka huu wa 2024 yamekamilika.
Tamasha hilo litafanyika katika viwanja na kumbi za Taasisi (TaSUBA – Bagamoyo) katika mji wa kihistoria wa Bagamoyo, Tanzania.
Mkuu wa Chuo TaSUBA, Dk Herbert Francis Makoye amesema Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ni tukio la kipekee na lenye vitu vya kuvutia.
Dk Makoye amesema tamasha hilo linahusisha aina mbalimbali za sanaa ikiwemo muziki wa asili na kisasa, ngoma, maigizo, sarakasi, vichekesho, mazingaombwe, mashairi, maonesho (exhibition) na sanaa zingine.
“Tamasha hilo pia linatoa jukwaa la kipekee kwa wasanii wa ndani na kimataifa kushirikiana na kubadilishana uzoefu na ujuzi na wasanii wanaotakiwa katika tamasha hilo ni waimbaji, wanamuziki, wachekeshaji, sanaa za ufundi, wachoraji, wachonga sanamu na wataalamu wengine wa ubunifu,” amesema Dk Makoye.