BurudaniFilamu

Forrest Gump

NI kupiga soga kwa kwenda mbele…Forrest Gump anasimulia hadithi ya maisha yake kwa
watu waliokaa karibu naye kwenye benchi huko Savannah, Georgia mwaka 1981.

Katika siku yake ya kwanza shule, Greenbow huko Alabama, kijana mdogo Forrest Gump anakutana na msichana wa rika lake aitwaye Jenny Curran. Licha ya uwezo wake mdogo
akili, lakini uwezo wake wa kukimbia unamfanya kupata nafasi ya masomo kupitia soka.

Waliosema hayawi sasa yanakuwa. Forrest Gump anahitimu chuo na kisha anajiunga na jeshi, ambapo anampata rafiki, askari mwenzake aitwaye Bubba. Ni huyu Bubba anamshawishi Forrest Gump kufanya biashara ya uduvi (dagaa kamba) vita vikiisha.

Wanakwenda vitani Vietnam, huko wanashambuliwa na Bubba anauawa katika mapigano dhidi ya vikosi vya Vietnam. Forest Gump anafanikiwa kuwaokoa askari wengi wa kikosi chake, ikiwa ni pamoja na Luteni wake, Dan Taylor, ambaye licha ya kupona lakini anapoteza miguu yake yote.

Licha ya Forrest Gump kujeruhiwa kwa risasi kwenye makalio, anapata tuzo ya ‘Medal of Honor’ kwa ujasiri wake baada ya vita kwisha. Wakati Forrest Gump akitibiwa jeraha la risasi kwenye makalio yake, anagundua kuwa ana kipaji katika mchezo wa ‘ping pong’.

Anapata umaarufu kwa kucheza mchezo huo. Katika mkutano unaofanyika jijini Washington D.C, Forrest Gump anaungana tena na mwanadada Jenny Curran. Anaporudi nyumbani,
Forrest Gump anatumia mapato aliyopata kununua boti ya kuvulia uduvi, akijaribu kutimiza ahadi yake kwa rafiki yake Bubba.

Baadaye anaungana tena na Luteni Dan, na siku moja kimbunga Carmen kinapiga baharini na kuharibu boti zote isipokuwa boti yao pekee na wao wanapata kiasi kikubwa sana cha uduvi.

Forrest Gump anatumia mapato yake kununua meli kubwa ya kuvulia uduvi. Luteni Dan anawekeza katika kampuni ya Apple Computer, kampuni ambayo Forest Gump anadhani ni ya kuuza matunda.

Kisha Forest Gump anarudi nyumbani kumwona mama yake katika siku zake za mwisho…
Kuna mengi sana ya kujifunza katika filamu hii ya dakika 142, ikiwemo historia na utamaduni wa Marekani.

Hadithi yake inaelezea mambo yaliyotokea kwenye miongo kadhaa katika maisha ya Forrest Gump, mtu aliyekuwa na akili ndogo, akili iliyo chini ya kiwango cha kawaida (IQ 75) lakini aliyejaliwa moyo-mzuri, huruma na shujaa wa Alabama, ambaye anashuhudia
baadhi ya matukio ya nusu ya mwisho wa Karne ya 20 huko Marekani; hasa, kipindi cha kati cha kuzaliwa kwake mwaka 1944 na 1982.

Nilipoitazama filamu hii ya Forest Gump kwa mara ya kwanza kabisa haikunivutia,
nadhani ni kwa sababu wakati huo sikuwa makini. Lakini nilipoitazama tena nikagundua kuwa ni ‘bonge la movie’.

Kwa kifupi filamu hii inafundisha mengi kuhusu maisha na maana ya maisha. Kwamba maisha si mabaya kama ambavyo watu wengi wanataka yaonekane. Kwamba kijana asiye na hatia anaweza kufanikisha maisha ya wengi kwa hali yake.

Na kama hujawahi kuitazama au uliitazama lakini hukuipenda nakushauri uitazame tena. Ukweli inastaajabisha sana… ni moja ya sinema bomba sana, na kwa kweli ilistahili kuzoa
tuzo nyingi kama ilivyotokea baada ya kutoka kwake.

Mwaka 1995 ilishinda Tuzo sita za Oscar (Academy Awards) kwenye vipengele vya: Sinema Bora; Mwongozaji Bora (Robert Zemeckis); Mwigizaji Bora (Tom Hanks); Script Bora iliyotokana na Riwaya (Eric Roth); Best Visual Effects; na Filamu iliyohaririwa vizuri.

Pia ilipata tuzo nyingine nyingi na kuteuliwa katika tuzo kibao, ikiwa ni pamoja na Golden Globes, People’s Choice Awards na Young Artist Awards, kati ya nyingi nyingine.

Mwanzoni waongozaji wawili walipewa fursa ya kuiongoza filamu hii kabla hajachaguliwa Robert Zemeckis huku Terry Gilliam akikataa ofa hii. Barry Sonnenfeld aliunganishwa kwenye filamu hii lakini aliondoka kwenda kuongoza filamu ya Addams Family Values.

Forrest Gump ni filamu ya mwaka 1994 iliyotolewa rasmi Julai 6, 1994. Inatokana na riwaya yenye jina hilo hilo iliyoandikwa na Winston Groom mwaka 1986.

Baada ya kutoka ilipata mafanikio makubwa kibiashara kwa kazi zote zilizotoka mwaka huo, na kuwa sinema ya kwanza iliyofanikiwa sana ya kampuni ya Paramount Pictures tangu iungane na Viacom.

Hadi sasa imeshaingiza zaidi ya dola za Marekani milioni 678.2. Picha za sinema hii zilipigwa mwishoni mwa mwaka 1993, hasa katika maeneo ya Georgia, North Carolina na
South Carolina.

Mwaka 1996, mgahawa bora wa ‘Bubba Gump Shrimp Company’ ulifunguliwa kutokana na
filamu hii na tangu wakati huo umeenea maeneo mengi duniani. Mnamo 2011, Maktaba ya
Congress iliihifadhi filamu hii kwa Msajili wa Taifa wa Filamu za Marekani kama “kumbukumbu ya kiutamaduni na kihistoria kwa taifa la Marekani.”

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button