Willy Paul aweka wazi kilichomkosesha Kolabo kwa Wizkid
NAIROBI: MWANAMUZIKI kutoka Kenya Willy Paul ameweka wazi sababu iliyomfanya ashindwe kurekodi wimbo wa kushirikiana na mwanamuziki wa Nigeria Wizkid miaka minne iliyopita akidai ilitokana na taarifa potofu zilizoenezwa kuhusu wasanii wa Kenya kwenye muziki kimataifa.
Willy Paul amesema watu wanaosambaza taarifa hizo potofu ni miongoni mwa wanamuziki na wadau wa muziki wa Kenya lakini hakuwa tayari kuwaweka wazi watoa taarifa hao potofu zaidi ya kusema kwamba waliopotosha kuhusu yeye na muziki wa Kenya kimataifa wanajijua wenyewe na hana haja ya kuwataja.
Msanii huyo anayetamba na wimbo wake mpya wa ‘Kuukuu’ ambao umepokelewa vyema nchini Kenya ameongeza kwa kulalamikia baadhi ya wasanii mahiri wa Kenya kutopewa thamani yao jambo ambalo linaua tasnia ya muziki wa Kenya.
“Wasanii wengi wa Kenya wamekithiri tu lakini hawatambuliki na hawapewi thamani,jambo ambalo linalua tasnia ya muziki”, amesema Willy.
Mashabiki wake wengi walionekana kuguswa na hisia zake na wengi walijumuika katika ukurasa wake wa Instagram wakiandika kuhusu kilichomtokea kwa miaka minne iliyopita.
Baada ya taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Saldido International Entertainment aliwataka Wakenya kutanguliza talanta na ustadi badala ya umaarufu wao, akiwataka wakome kusifu kejeli zinazowekwa mitandaoni ama kuzungumzwa kokote bali waunge mkono vipaji vya kweli ili kuinua muziki wa Kenya.