‘Sitarajii kuwa na watoto na Zari’ – Mume wa Zari
KAMPALA: MUME wa mfanyabiashara Shakib Cham amefunguka kuwa hatarajii kupata watoto na mkewe, Zari Hassan kwa madai ya umri wake.
Katika rekodi ya sauti ya hivi majuzi ambapo alizungumza kwa lugha ya Kiganda, Shakib alisema, “Sitarajii kuwa na watoto naye. Yeye yuko katika umri ambao kuwa na watoto hauwezekani tena. Nina Watoto nachofanya ni kumpendeza na kumpenda.”
Shakib alifichua kuwa kumuoa Zari kumemletea umaarufu na changamoto, ikiwemo kukosa heshima. Kauli yake inakuja siku chache baada ya Zari kutishia kutafuta mtu mwingine baada ya kutofautiana na mume wake huyo kutokana na ujio wa msanii Diamond Platnumz nyumbani kwake nchini Afrika Kusini aliyekwenda kwa ajili ya sherehe ya kuzaliwa kwa binti yao.
“Ikiwa mtu wangu hataki kunitambua mimi ni nani, ni aibu! Hakika nitapata mtu ambaye atathamini thamani yangu. Nina thamani kubwa zaidi,” Zari alisema. Alisema zaidi, “Ikiwa hautatambua thamani yangu, nitatafuta mtu wa kuchukua nafasi yako.”
Juzi, Zari pia alipendekeza kwamba ikiwa Shakib atatafuta mke wa pili, naye anaweza kufikiria kuwa na mume wa pili. “Nchini Afrika Kusini, tunaweza kuwa na waume wawili; ni sheria mpya hapa. Ukipata mtu mwingine, naweza pia kupata mume wa pili,” alisema kwenye chaneli yao ya pamoja ya YouTube.
Akimzungumzia Shakib, Zari alimkumbusha juu ya haki yake akiwa Muislamu ya kuoa hadi wake wanne, huku akimkumbusha kuwa naye kama mkazi wa Afrika Kusini anaweza kuwa na waume wawili.
Zari aliibua mada hii baada ya kumshuku Shakib kwa kuonyesha kuvutiwa na wanawake wengine kupitia ujumbe.