
DAR ES SALAAM: UONGOZI wa klabu ya Simba umetangaza kauli mbiu mpya, “Hii Tunavuka,” kuelekea mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, utakaochezwa Aprili 9.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kauli mbiu hiyo inalenga kuongeza hamasa kwa wachezaji na mashabiki wa timu hiyo.
“Pamoja na kuwepo kwa kauli mbiu inayofanya vizuri sana Tanzania ya ‘Ubaya Ubwela,’ mechi hii ya marudiano tunakuja na kauli mbiu mpya, Hii Tunavuka. Kwa misimu mitano mfululizo tumekuwa tukiishia robo fainali, lakini safari hii, kwa mapenzi ya Mungu, tunavuka kwenda nusu fainali. Hii inapaswa kuingia akilini kwa kila mchezaji na kila shabiki wa Simba,” amesema Ahmed.
Ahmed ameongeza kuwa kikosi cha Simba kitaondoka nchini alfajiri ya Machi 28 kuelekea Misri. Wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars wataungana na wenzao nchini Misri.
“Moussa Camara na Steven Mukwala tayari wamewasili nchini kujiunga na wenzao kwa maandalizi ya safari. Pamoja na mipango tuliyonayo, tunapaswa kujipanga na kujiandaa kwa sababu tunakabiliana na timu kutoka Misri, taifa lililoingiza timu nne kwenye robo fainali za michuano ya Afrika,” amesema Ahmed.
Amesisitiza kuwa Simba inaingia katika mchezo huo ikitambua ugumu wake lakini ikiwa na dhamira thabiti ya kufuzu kwa nusu fainali.
Kuhusu Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa, Ahmed amewatoa mashaka mashabiki wa Simba kwa kusema kuwa uwanja huo umeshafanyiwa ukaguzi.
“Majibu rasmi bado hayajatoka, lakini mazungumzo yanaonyesha kuwa kuna maboresho makubwa kwenye uwanja huo ukilinganisha na mara ya mwisho ulipokaguliwa. Hivyo, nafasi ni kubwa ya kucheza mechi hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa,” amesema.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa maandalizi yanaendelea kwa nguvu zote ili kuhakikisha Simba inapata ushindi na kufanikisha ndoto ya kufika nusu fainali.