Simba, Yanga zilitisha 2024!

DAR ES SALAAM: MWAKA 2024, Tanzania iliandika historia nyingine katika soka la Afrika baada ya kuwa nchi pekee iliyokuwa na timu bili kwenye robo fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya timu hioz kuishia katika hatua hiyo.
Timu za Simba na Yanga ndizo zilizoipeperusha bendera ya taifa kwa katika michuano hiyo ambapo mbali na heshima hiyo ni kwa mara ya kwanza timu hizo kufuzu kwa pamoja katika hatua ya makundi ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa na robo fainali ya michuano hiyo.
Hivyo tunaweza kusema mwaka 2024 ulifungua ukurasa mwingine wa soka katika ngazi ya klabu, kufikia mwaka 2024 Simba ilikuwa imejipambanua vyakutosha kwenye michuano hiyo ikifuzu mara kadhaa kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo lakini kwa Yanga ilikuwa ni hadithi ya tofauti kwani walisubiri kwa kipindi cha miaka 25 ndipo wakatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Yanga walirejea kwa kishindo baada ya unyonge wa miaka 25 ambapo walikuwa gumzo kote barani Afrika hasa kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ulioamuliwa kwa mikwaju ya penalti baada ya kukoseka na bao katika dakika 180 za mchezo huo.
Mchezo baina ya timu hizo ulitawaliwa na maamuzi yenye utata yakiwachanganya wanazi wa soka Afrika wengine wakiamini Yanga walistahili kupata bao kwenye mchezo ule lakini mwamuzi hakuwa makini.
Kwa upande wa Simba waliishia pia katika hatua ya robo fainali kwa kupoteza kwa jumla ya mabao 3-0 kutoka kwa mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo Al Ahly ya Misri.
Licha ya timu hizo kushindwa kusonga mbele Tanzania ilijivunia ushiriki wao kwani ziliongeza pointi katika msimamo wa CAF hivyo kuiweka salama nafasi ya taifa kuwa na timu nne kwenye michuano hiyo. Mwaka 2024 Simba na Yanga walitisha sana Kimataifa je watalifanikisha tena hilo kwa mwaka 2025? Karata ipo mikononi mwao.