Simba kwenda kujiuliza tena Misri
DAR ES SALAAM: WAKATI Simba wakiendelea kufanya maboresho ya kikosi, timu hiyo inatarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi Juni na wanatarajia kwenda nchini Misri kwa ‘Pre Season’ ya msimu wa 2024\25.
Imeelezwa kuwa licha ya uongozi wa klabu hiyo ukiendelea kuwapa ‘THANK YOU’ baadhi ya wachezaji wao, tayari wameshachagua nchi ambayo wataenda kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano wanayoshiriki.
Taarifa zilizoifikia Spotileo kuwa viongozi waliangalia nchi gani ambayo wanaweza kwenda kwa ajili ya timu hiyo kupata mazingira mazuri ya kufanya maandalizi ya msimu mpya na Misri ni nchi iliyopita kwa timu hiyo kwenda kuweka kambi.
“Viongozi wako makini kujenga timu katika usajili lakini pia wameangalia nchi gani timu itaenda nchi gani kuweka kambi, kutokana na urafiki uliojengwa na Al Ahly wameona waende nchini Misri kutokana na mazingara mazuri na kuweza kupata timu za kucheza mechi ya kirafiki kipindi watakachokuwa nchini humo,” amesema kigogo huyo ndani ya Simba.
Katika hatua nyingine Simba imetangaza kuachana na beki wa kati, Kennedy Juma ambaye hatokuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kuelekea msimu mpya baada ya mkataba wake kufikia tamati.
Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally amesema kila kitu kinaenda kwa mpangilio wanaendelea na kutoa ‘THANK YOU’ kwa wachezaji ambao hawapo kwenye mipango ya timu msimu ujao.
Amesema baada ya kufanikiwa kuwaaga baadhi ya wachezaji ambao watakuwa kwenye mipango yao, wataweka wazi mipango mwingine ikiwemo suala la kambi wataweka wapi na watakaa muda gani.
“Wanasimba wanatakiwa kukaa mkao wa kula maana yanayokuja yanafurahisha kwa sababu tayari usajili wa wachezaji wapya umeshaanza kufanyika na unaendelea kuimarisha kikosi kwa kuleta vyuma vingine,” amesema Ahmed.
Amesema leo wameendelea na utaratibu wa kuacha wachezaji na leo imekuwa zamu ya beki wao, Kennedy Juma ambaye amedumu miaka mitano ndani ya klabu hiyo na hatokuwa sehemu ya timu kuelekea msimu mpya baada ya mkataba wake kufikia tamati.
Kennedy alijiunga Simba Julai, 2019 akitokea Singida United na amekuwa akifanya vizuri uwanjani kila anapopata nafasi ya kucheza ndani ya timu hiyo, ni mmoja ya wachezaji watulivu na wasikivu ndani ya kikosi cha Simba amekuwa akifanya kila anachotakiwa ndani ya muda unaohitajika.
Pamoja na ubora na uwezo alionao Kennedy lakini hayupo kwenye mipango ya kusuka kikosi imara kuelekea msimu ujao wa mashindano hali ambayo hawakumuongezea mkataba.