Simba kuhamishia vita yao kwa Greenland leo

DAR ES SALAAM: TIMU ya soka ya Simba leo inaanza rasmi kampeni ya michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa kumenyana na Greenland katika mchezo utakaochezwa saa moja usiku kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Wekundu wa Msimbazi wanaingia kwenye mashindano hayo wakiwa na morali kubwa baada ya kutoka kushinda bao 1-0 dhidi ya Stade Malien katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, licha ya kuaga michuano hiyo.
Ushindi huo ulitokana na muunganiko mzuri wa kikosi pamoja na ari ya kupambana kwa wachezaji, jambo ambalo benchi la ufundi limeahidi kuendelea kuliboresha ili kupata matokeo chanya katika mashindano ya ndani.
Kocha Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema mchezo wa leo ni muhimu kwa timu yake kuanza kwa ushindi ili kuweka mazingira mazuri ya kutwaa taji hilo.
“Ni mashindano muhimu kwetu, tunahitaji kuanza kwa nguvu na kupata ushindi. Wachezaji wako kwenye hali nzuri na wameonesha kiwango bora katika mchezo uliopita,” amesema Barker.
Mbali na mchezo huo, ratiba ya Kombe la Shirikisho la CRDB leo pia itashuhudia KMC ikimenyana na Bandari ya Tanzania katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku kila timu ikisaka kusonga mbele katika michuano hiyo.




