Shime:Twiga Stars inajiandaa na hatua inayofuata

DAR ES SALAAM: KOCHA wa timu ya Taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, Bakari Shime, amesema kikosi chake kimepata nafasi nzuri ya kujiandaa kwa hatua inayofuata ya mbio za kufuzu Olimpiki za Los Angeles 2028 baada ya kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano dhidi ya Botswana.
Twiga imefuzu hatua ya pili baada ya kuiondosha Botswana kwa jumla ya mabao 7-1, ugenini ikishinda bao 1-0 na nyumbani 6-0.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Shime amewapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri waliyoifanya, akieleza kuwa katika kipindi cha pili timu yake iliboresha umiliki wa mpira na kujenga mashambulizi kuanzia safu ya nyuma, tofauti na kipindi cha kwanza ambacho walipata changamoto katika eneo hilo.
Amesema mabadiliko hayo yaliisaidia Twiga Stars kucheza kwa utulivu zaidi, kumiliki mpira kwa muda mrefu na kutumia nafasi zilizopatikana kufunga mabao.
Shime ameongeza kuwa kikosi chake sasa kinaelekeza nguvu katika maandalizi ya hatua inayofuata, ambapo kinatarajiwa kukutana na mshindi kati ya Ethiopia na Rwanda.
Amesema benchi la ufundi litaifuatilia timu itakayokuwa mpinzani wao ili kubaini maeneo muhimu ya kujiandaa nayo na kuhakikisha Twiga Stars inaingia katika hatua hiyo ikiwa tayari kwa ushindani zaidi.




