Nyumbani

Shime aomba radhi Watanzania

KUFUATIA kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Zambia kilichopata timu ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Bakari Shime, ameomba radhi kwa Watanzania kwa matokeo hayo mabaya.

Shime amesema timu yake ilianza kupoteza mwelekeo baada ya mchezaji wake, Lydia Kabambo, kuumia na kutolewa nje. Juhudi zao za kutafuta mbadala zilitoa nafasi kwa Zambia kufunga bao la uongozi.

Ameeleza kuwa baada ya bao hilo, Zambia walipata kujiamini na kuanza kumiliki mpira, hasa kipindi cha pili, na baadaye wakafunga mabao mengine mawili kutokana na makosa ya Serengeti Girls, hali iliyowafanya washindwe kurejea mchezoni.

“Pole kwa Watanzania wote, matarajio hayakuwa haya. Tulitarajia kucheza vizuri na kupata matokeo. Kipindi cha kwanza tulidhibiti mchezo na kutengeneza nafasi, lakini hatukuzitumia. Pia, tulilinda vizuri, hakukuwa na hatari yoyote,” amesema Shime.

Amesema atafanyia kazi mapungufu ili katika mchezo wa marudiano waweze kufanya vizuri.

Kwa upande wa Zambia, Kocha Mkuu Carol Kanyemba amesema ushindi wao ulitokana na kumweka Mungu mbele kwa kila jambo, pamoja na juhudi za wachezaji wake zilizowasaidia kupata matokeo mazuri.

Amewapongeza wachezaji wake kwa nidhamu waliyoonesha uwanjani, akisema walipambana na kupata ushindi. Kuhusu mchezo wa marudiano utakaochezwa Zambia, Kanyemba amesema hawataenda kulala, bali watahakikisha wanatumia vyema uwanja wao wa nyumbani kufunga mabao mengi na kusonga mbele hatua inayofuata.

Tanzania na Zambia zitakutana tena Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola, ambapo mshindi wa mechi hiyo atakutana na kati ya Benin au DR Congo kwenye hatua inayofuata.

Related Articles

Back to top button