Sanaa za uoni zaiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia

KENYA: Sanaa za uoni/ufundi ni miongoni mwa sekta chache nchini Tanzania na duniani zinazochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya urithi wa sanaa ya kipekee unaoitangaza nchi kimataifa.
Akizungumza na Spoti Leo baada ya kuwasilisha mada katika kongamano la The East African Art Nexus (TEANEX) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Msanii Safina Kimbokota amesema kuwa sanaa za uoni nchini Tanzania zimekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza urithi wa kipekee unaotambulika duniani.
Amesema sanaa hizo zimeiwezesha Tanzania kujijengea jina kimataifa kupitia ubunifu na utofauti wa kazi zinazozalishwa na wasanii wake.
Akifafanua zaidi, Kimbokota amezungumzia aina mbili kuu za sanaa za uoni/ufundi zinazotambulika sana:“Aina ya kwanza ni Sanaa ya Tingatinga, ambayo kwa sasa ipo chini ya Tingatinga Arts Cooperative Society.
“Ilianzishwa na wasanii sita mwaka 1990 kwa lengo la kuendeleza urithi wa mwanzilishi wake, Edward Saidi Tingatinga,” amesema.
Ameeleza kuwa sanaa hiyo, inayotambulika kwa matumizi ya rangi kali pamoja na michoro ya wanyama, miti na maisha ya binadamu, imekuwa nembo (brand) kubwa ya sanaa ya Tanzania duniani.
“Kwa sasa, kuna maelfu ya wasanii ndani na nje ya nchi wanaotegemea sanaa hii kwa maisha yao. Kazi zao zinauzwa katika masoko ya Ulaya, Marekani na Japan kwa thamani kubwa,” ameongeza.
Aidha, Safina amesema sanaa ya Tingatinga imetoa ajira kwa vijana wengi Afrika Mashariki na hata katika mabara mengine, hasa kutokana na ukuaji wa sekta ya utalii.
Kuhusu aina ya pili, Kimbokota ametaja vinyago vya Kimakonde vinavyotengenezwa kwa kutumia mti wa mpingo.
“Vinyago vya Kimakonde ni urithi wa karne nyingi kutoka mkoa wa Mtwara, na vimetambuliwa na UNESCO kama urithi wa utamaduni usioshikika,” amesema.
Amefafanua kuwa vinyago hivyo hujumuisha maumbo mbalimbali kama Ujamaa, Shetani, Mawingu na Binadamu, na vinapatikana katika makumbusho makubwa duniani ikiwemo British Museum.
Kwa upande wa mafanikio ya kiuchumi, amesema “Biashara ya vinyago hivyo imekuwa ikichangia mapato makubwa ya fedha za kigeni nchini, huku pia ikisaidia kulinda misitu ya mpingo kupitia matumizi endelevu ya malighafi hiyo.”amesema Safina
Kwa ujumla, sanaa za uoni zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi, utamaduni na utambulisho wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa.




