Saidi Chino, Ibrahim Mafia ulingoni wikiendi hii
DAR ES SALAAM: MABONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Ibrahim Mafia na Saidi Chino kutoka Kampuni ya Mafia Boxing Promotion kupanda ulingoni mapambano ya kimataifa yatakayochezwa Jumamosi ya wikiendi hii, Ukumbi wa City Centre uliopo Magomeni Sokoni jijini.
Ibrahim atacheza na Prasitsak Phaprom wa Thailand pambano lisilo la ubingwa raundi nane uzito wa kati (KG 53) Said Chino (kilo 59) akitarajia kumvaa Simpiwe Vityeka wa Afrika Kusini.
Mkurugenzi msaidizi wa Mafia Boxing Promotion, Ally Zayumba alisema pambano hilo la kimataifa litakuwa na mapambano 15 huku nane kati ya hayo yakiwa ni ya kimataifa.
“Maaandalizi yanaendelea vizuri mpaka sasa kila kitu kimekamilika, mabondia wote wapo sawa kwa lengo la pambano letu la kimataifa ambalo tumeliita ‘The One’, mabondia wetu watacheza na mabondia kutoka mataifa tofauti.
“Kikubwa ni kwamba siku ya Ijumaa kutakuwa na zoezi la kupima uzito katika eneo la Magomeni Sokoni, tunawakaribisha wadau na mashabiki wangu na tiketi za pambano zitapatikana siku hiyo kwa kiiingilio cha shilingi 20,000 na 10,000 kawaida, tumeweka kiingilio kidogo ili kutoa fursa ya mashabiki wengi kujitokeza,”alisema Zayumba
Pambano la utangulizi yatakuwa kati ya Richard Mtangi akitarajia kucheza dhidi ya Magambo Christopher huku Salmin Kasim akipewa Abert Kimario kutoka Kenya.
Wengine ni Yohana Mchanja yeye anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Joseph Akai, Ramadhan Ramadhan akitarajia kumvaa Guy Tshimanga wa DR Congo huku Ramadhan Kimoko akipewa Harvey Mkacha wa Malawi.