Fury amuonya mwanawe Prince John

BANGKOK: BINGWA wa zamani wa ngumi wa uzito wa juu duniani, Tyson Fury amesema mwanawe mkubwa, Prince John James, ana ndoto ya kufuata nyayo zake na kuwa bondia wa kulipwa siku za usoni.
Fury, ambaye ni baba wa watoto saba, amesema mwanawe huyo mwenye umri wa miaka 15 tayari ameanza kujifunza masuala ya ndondi na kwa sasa yupo naye kambini nchini Thailand wakijiandaa na pambano lake la kurejea ulingoni dhidi ya Arslanbek Makhmudov litakalopigwa Aprili 11 mwaka huu.
Akizungumza na jarida la The Ring, Fury amesema anaamini mwanawe ana nia ya dhati ya kuwa bondia, lakini anafahamu kuwa watoto wa mabondia maarufu hukumbana na shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki na wachambuzi wa mchezo huo.
“Nadhani ataingia kwenye ndondi kwa asilimia mia moja. Hicho ndicho anachotaka kufanya na ndiyo maana yupo kambini akifanya mazoezi. Hata hivyo tunajenga hatua kwa hatua,” amesema Fury.
Amesema kuwa watoto wa mabondia maarufu mara nyingi hukumbwa na ukosoaji mkali, wakilinganishwa na mafanikio ya wazazi wao.
Fury alitolea mfano wa Campbell Hatton, mwana wa bondia nguli Ricky Hatton, ambaye alisema alipata shinikizo kubwa kutokana na kulinganishwa na baba yake aliyekuwa nyota mkubwa wa ndondi.
Kutokana na hali hiyo, Fury amesema anataka mwanawe awe tayari kikamilifu kabla ya kuanza kupigana rasmi ili kukabiliana na changamoto hizo.
Mbali na mwanawe, pia ameambatana na mpwa wake John Boy Fury kambini Thailand na amesema mbali na kuwafundisha ndondi, anawajenga pia kisaikolojia na kitabia.



