Ratcliffe awajia juu mastaa wa Manchester United

MANCHESTER:MMILIKI mwenza wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe, amesema baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo hawana viwango vya kucheza hapo, huku wengine wakilipwa mishahara mikubwa isiyoendana na uwezo wao uwanjani.
Ratcliffe aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na mwandishi Dan Roan wa BBC Sport, ambapo alieleza kuwa wachezaji hao wanaiingiza klabu hasara, hivyo kuna haja ya kubuni mbinu za kubana matumizi.
Akizungumzia viwango vya kiungo Casemiro, mshambuliaji Rasmus Højlund, kipa André Onana, na mawinga Antony (Real Betis kwa mkopo) na Jadon Sancho ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Chelsea kwa mkopo, bilionea huyo alibainisha kuwa wachezaji hao walirithiwa na uongozi wake mpya, jambo linaloonekana kama hatua ya kukwepa lawama juu ya viwango vyao.
“Baadhi ya wachezaji wetu si wazuri, hawana viwango vya kuifaa Manchester United, na wengine wanalipwa fedha nyingi kupita kiasi. Lakini ni kazi yetu kujenga kikosi chenye uwajibikaji, ingawa itachukua muda,” alisema Ratcliffe.
Kauli yake inakuja siku moja baada ya mashabiki wa Manchester United kuandamana katika mchezo waliopoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Arsenal, wakipinga umiliki wa klabu hiyo na kuutaja kama chanzo cha anguko la timu msimu huu.
Manchester United kwa sasa wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 34 baada ya michezo 28, wakishinda mechi 9, kutoka sare 7, na kupoteza mara 12. Matokeo haya yamesababisha pengo la pointi 36 kati yao na vinara wa ligi hiyo, Liverpool.