Rapa CMB Prezzo, ageukia muziki wa Injili

RAPA kutoka nchini Kenya, Jackson Ngechu, maarufu kwa jina la CMB Prezzo amezua maswali mengi kama ameachana na muziki wa kidunia ama la baada ya kuonekana akiimba wimbo wa injili katika Kanisa la Empowerment Christian Church (ECC) Jijini Nairobi hivi karibuni.
Prezzo aliimba wimbo wake huo wa Injili ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu kubadilika kiimani mbele ya mchungaji na waumini wa kanisa hilo waliojawa na furaha kumsikia rapa huyo wimbo wake wa dini.
Mchungaji Natasha alimpongeza Prezzo: Hongera sana Mwanangu wa Kiroho @prezzo254 kwa kuachia wimbo wako mpya wa Injili uliozinduliwa leo @eccnairobi. Mungu akutumie kuwafikia vijana wetu. Kizazi chetu ni jukumu letu. Ninajivunia wewe, mwanangu.”
Katika ibada hiyo, Prezzo alionyesha safari yake ya kiroho, akikaribishwa kwa uchangamfu na waumini alipoanza njia mpya ya Imani tofauti na alivyokuwa akiimba muziki wa kidunia.
Akiwa ameongozana na mama yake, baadaye aliungana na Mchungaji Natasha ofisini kwake kwa maombi na majadiliano ya kina.
Prezzo alisahini kitabu cha wageni cha kanisa hilo, kuashiria kujitolea kwake. Akitafakari juu ya Imani yake, alishukuru kwa makaribisho hayo mazuri, huku akiamini alichofanya ni kitu sahihi akijifananisha na mbegu.