Muziki

Smart Boy aibuka mshindi wa kwanza gospel singeli

DAR ES SALAAM: kwa mara ya kwanza katika historia ya tuzo za muziki wa Injili nchini Tanzania, muziki wenye vionjo vya singeli umejishindia tuzo kupitia msanii wa injili Emmanuel Peter ‘Smart Boy’.

Ushindi huu umetokea kwenye tuzo za mwaka huu za Muziki wa Nyimbo za Injili Afrika Mashariki (EAGMA), na hivyo kuweka historia mpya ya mchanganyiko wa muziki wa Injili na singeli katika jukwaa kubwa la kimataifa.

Akizungumza katika hafla maalum ya kutangaza mshindi huyo pamoja na kufunga rasmi msimu wa tuzo za EAGMA 2025, Ofisa Mtendaji Mkuu wa tuzo hizo, Magreth Chacha amesema taasisi yao imetambua mchango mkubwa wa muziki wa injili wenye mahadhi ya singeli katika kueneza neno la Mungu, hivyo kuamua kuutambua rasmi kupitia tuzo.

“Siku ya leo nina mambo matatu muhimu kwanza ni kutoa shukrani kwa wadau wote waliotuunga mkono kufanikisha tuzo hizi katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Pili, ni kutangaza mshindi wa kipengele cha Gospel Singeli, ambapo ushindani ulikuwa mkali kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Smart Boy kupitia wimbo wake ‘Singeli ya Yesu’, Boni Mwaitege (Pesa), Pius Wilson (Mchungaji Wangu), Deliv Shuma (Mbingu Zimefunguka), Survival Gospel Choir (Waharibie), na Kibonge wa Yesu (Kibonge wa Yesu). Smart Boy ameibuka mshindi kwa kura nyingi zaidi,” amesema Magreth.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, tuzo za mwaka huu zilivutia washiriki na mashabiki wengi kutoka Kenya, Uganda na Rwanda, huku jumla ya tuzo 56 zikitolewa.

Ameahidi kuwa toleo la 2026 litakuwa kubwa zaidi, likihusisha maboresho ya vipengele na mchakato wa tuzo kwa ujumla.

“Tuzo za mwaka 2026 tunatarajia kuanza mapema maandalizi. Tutatoa ratiba ya nchi tutakazoanzia na kumalizia.

Lengo letu ni kukuza muziki wa injili, kuwahamasisha wasanii na kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa njia ya muziki,” ameongeza.

Kwa upande wake, Smart Boy mara baada ya kupokea tuzo hiyo ameeleza kuwa amepata hamasa kubwa ya kuendelea kuboresha kazi zake za muziki wa Injili.

Alitoa shukrani kwa waandaaji wa EAGMA na kueleza kuwa ushindi huo ni chachu ya kufanikisha lengo lake la kulitangaza neno la Mungu kupitia miondoko ya Gospel Singeli.

“Tuzo hii si yangu peke yangu, ni ya mashabiki wote na watu wanaoamini kuwa Injili inaweza kufika popote – hata kwenye singeli. Nimehamasika zaidi kuendelea kufanya kazi bora kwa ajili ya utukufu wa Mungu,” amesema Smart Boy

Related Articles

Back to top button