Ligi Kuu

Ramovic:Yanga ya sasa haina ‘Superstar’

DAR ES SALAAM: WAKATI Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wakitarajiwa kushuka dimbani dimbani kesho dhidi ya Mashujaa FC, Kocha wa timu hiyo,Sead Ramovic amesema wanaingia katika mchezo huo na kitu kipya ikiwemo kutokuwa na mchezaji mkubwa kuliko wengine ndani ya kikosi chake.

Yanga wanashuka dimbani kesho katika mchezo huo wakiwa nyumbani Uwanja wa KMC uliopo Mwenge ikiwa ni mechi ya kwanza kuutumia uwanja huo baada ya kuondoka Azam Complex.

Ramovic amesema mchezo wa kesho utakuwa wa kipekee, hakuna mchezaji mkubwa ndani ya timu, anahitaji watu wenye njaa ya kufunga na kuhitaji alama tatu dhidi ya Mashujaa.

“Nahitaji timu bora na sio mchezaji mmoja, kama hatojituma uwanjani hata kama ni mzuri kwangu hana nafasi. nyakati mbaya hazidumu siku zote ila tunahitaji kubadilika kuanza namna ya kuwaza hadi namna ya kuukabili mchezo,” amesema.

Ramovic amesema maandalizi yameendelea vizuri, hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu Mashujaa FC, wana wachezaji na benchi la ufundi na watacheza kwa kuwaheshimu kutafuta pointi tatu muhimu.

Katika mchezo wa kesho Yanga watawakosa wachezaji  Djigui Diarra, Clatous Chama ambao walipata  majeraha katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, huku Aziz Andambwile na Chadrack Boka bado wakiukosa pia mchezo huo.

Related Articles

Back to top button