Muziki

Nandy afichua siri ya urafiki wake na Zuchu

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI Faustine Mfinanga ‘Nandy’, amefichua kuwa urafiki wake na msanii mwenzake wa muziki, Zuhura Othman ‘Zuchu’, si wa hivi karibuni kama baadhi ya mashabiki wanavyoweza kufikiri.

Nandy amesema urafiki wao ulianza muda mrefu na umeendelea kuimarika, licha ya kutokuwa rahisi kwa mashabiki kuwaona mara kwa mara wakiwa pamoja.

Amesema yeye na Zuchu wamekuwa wakikutana katika matukio mbalimbali ya nyuma ya kamera, ikiwemo studio, ambako wamekuwa wakizungumza na kushirikiana kama marafiki.

“Nandy na Zuchu hatuna bifu wala sababu ya kuwa na tofauti. Kila mmoja ana kazi yake na wote tumefanikiwa kupitia muziki ambao unatupatia kipato,” amesema Nandy.

Aidha, Nandy amesema waume zao, Diamond Platnumz na Billnass, ambao pia ni marafiki, wamekuwa sehemu ya kuhakikisha urafiki wao unaendelea kuwa mzuri kwa kuwasaidia kutokuwepo kwa sababu ya kugombanishwa.

“Waume zetu ni marafiki na wamekuwa wakihakikisha sisi pia tunaendelea kuwa na maelewano,” amesema.

Nandy na Zuchu waliwahi kushiriki pamoja katika shindano la kusaka vipaji vya kuimba kabla ya wote kupata umaarufu katika tasnia ya muziki.

Urafiki wao umeendelea kuonekana katika matukio mbalimbali, huku siku chache zilizopita wawili hao wakionekana pamoja katika hafla ya Henna Day ya Zuchu, ambapo walicheza na kufurahia muziki pamoja.

Related Articles

Back to top button