Ligi KuuNyumbani

Vichapo vimeondoka na makocha saba

LIGI Kuu Bara imeendelea kushika kasi wakati mabingwa wake Yanga wakiendelea kusalia kileleni mwa msimamo wakipania kutetea taji lao kwa mara ya tatu mfululizo.

Msimu huu kwenye Ligi Kuu hadi leo, makocha saba tayari wameachana na timu walizokuwa wakizifundisha.

Kila kocha ameondoka kwa sababu zake huku wengi wao walikuwa wakitimuliwa kwa
sababu ya mwenendo mbovu wa timu kwa kupata matokeo mabaya, huku wengine wakiondoka kwa kutofautiana na mabosi wao.

Kuna mambo mengi yanachangia hadi kutokea timuatimua, ikiwamo kutotimia kwa malengo licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa, hivyo viongozi kushindwa kuwa wavumilivu na matokeo hayo.

Gazeti la HabariLEO linakupa orodha ya makocha ambao hadi sasa wametimuliwa na  wengine kuachana na timu zao kwa sababu mbalimbali.

Hans van der Pluijm (Singida Fountain Gate)

Moja ya makocha wenye alama nzuri kwenye soka la Tanzania ni Mdachi huyu ambaye aliwahi kupita katika klabu ya Yanga na kuwapa makombe mawili ya Ligi Kuu Bara huku akisifika kwa soka safi la kampa kampa tena.

Baada ya kuwa na msimu mzuri wa 2022/23 na kuisaidia timu hiyo kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na kuweka rekodi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hiyo haikumzuia kuoneshwa mlango wa kutokea.

Matokeo yasiyoridhisha ya mwanzo wa msimu yalimuondoa kikosini na kumfanya aondoke mitaa ya Liti akiwa amedumu kwa msimu mmoja.

Ernest Middendorp (Singida Fountain Gate)

Alikuja kama mrithi wa Hans van der Pluijm katika kikosi cha Singida Big Stars, lakini ndiye
kocha aliyedumu kwenye timu hiyo kwa muda mfupi zaidi.

Aliiongoza Singida Fountain Gate kwenye mchezo mmoja pekee wa Kombe la Shirikisho Afrika ambao alishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Future ya Misri kisha akaoneshwa mlango wa kutokea.

Kocha huyo alidumu kama kocha wa Singida Fountain Gate kwa muda wa mwezi mmoja pekee.

Zuberi Katwila (Ihefu)
Alikuwa na mwendo wa kusuasua kwenye Ligi Kuu Bara lakini ushindi wa mabao 2-1 alioupata dhidi ya Yanga ulikuwa muhimu katika kulinda kibarua chake.

Upepo ulibadilika baada ya kupoteza michezo miwili dhidi ya KMC na Simba ikawa sababu
ya kutupiwa virago na walima mpunga hao kutoka Highland Estate.

Katwila anaondoka akiwa amedumu kwenye kikosi cha Ihefu kwa misimu mitatu Ligi Kuu
misimu miwili na Championship msimu mmoja.

Cedrick Kaze (NamungoFC)
Namungo walikuwa na matumaini makubwa na Kaze kutokana na kile alichokifanya akiwa na Yanga akisaidiana na Nassreddine Nabi ambao kwa pamoja walitwaa makombe sita ya ndani na kuifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Lakini wauaji hao wa Kusini walishindwa kupata kile walichotarajia kwa Kaze kwani katika
michezo sita ya kwanza ya Ligi Kuu, Namungo hawakupata ushindi kwenye mchezo hata mmoja, walipata sare tatu na kupoteza mechi tatu.

Hivyo walijikuta wakikusanya pointi tatu pekee, hivyo wakaamua kukaa mezani na kuvunja
mkataba na Kaze ambaye alidumu kama Kocha Mkuu kwa miezi minne.

Habibu Kondo(Mtibwa Sugar)
Wakata miwa wa Mtibwa Sugar baada ya misimu mitatu mfululizo kucheza michezo ya mtoano ili kubaki Ligi Kuu Bara iliamua kumshusha mitaa ya Turiani kocha Habibu Kondo.

Hakuwa na mwanzo mzuri na kujikuta akifungwa michezo mitatu na kupata sare mbili huku
akiwa amekusanya pointi mbili pekee katika michezo mitano.

Mwenendo huo haukuwaridhisha waajiri wake ambao walimuonesha mlango wa kutokea
akiwa amedumu katika kikosi hicho kwa miezi miwili pekee kuanzia Agosti hadi Oktoba.

Mwinyi Zahera(Coastal Union)
Timu ya Coastal Union ilikuwa na matumaini makubwa na Mwinyi Zahera wakiamini kuwa
anaenda kuwavusha kutoka sehemu moja hadi nyingine kutokana na uzoefu wake katika soka lakini mambo yakaenda ndivyo sivyo.

Katika michezo mitano ya awali alijikuta akiambulia pointi moja pekee baada ya kupata sare huku akipoteza michezo minne kitu ambacho hakikuwafurahisha waajiri wake ambao wakaamua kumbadilishia majukumu na kumpeleka kwenye timu za vijana.

Zahera amedumu katika kikosi cha Coastal Union kwa miezi mitatu pekee kuanzia Agosti hadi Oktoba, mwaka huu.

Robero Oliveira‘Robetinho’ (Simba)
Alikuwa na rekodi nzuri ya kucheza michezo 17 ya Ligi Kuu Bara bila kupoteza akishinda 16 na sare moja, lakini kichapo cha mabao 5-1 alichokipata kutoka kwa Yanga kimefuta kila kitu.

Robetinho ambaye ameiongoza Simba kushinda Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 3-1 safari imemkuta baada ya kipigo kizito cha mabao 5-1.

Related Articles

Back to top button