PSG yapewa nafasi kutwaa UCL

BUDAPEST: PARIS Saint-Germain (PSG) imepewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Arsenal kutokana na ubora wa kikosi chake pamoja na wachezaji wake kuwa na muda mkubwa wa kupumzika kabla ya fainali hiyo.
Takwimu zinaonesha kuwa wachezaji wa Arsenal wamecheza dakika karibu 7,000 zaidi katika mechi za ligi msimu huu ukilinganisha na PSG, jambo linalotajwa kuwaweza kuwapa faida mabingwa hao wa Ufaransa kuelekea mchezo wa mwisho wa michuano hiyo utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Puskas Arena mjini Budapest.
Kocha wa PSG, Luis Enrique, ametumia mfumo mkubwa wa mzunguko wa wachezaji katika michezo ya Ligue 1, akiwapumzisha nyota wake mara kwa mara ili kuwaweka fiti kwa mashindano ya Ulaya.
Nyota wa PSG kama Marquinhos, Ousmane Dembele na Khvicha Kvaratskhelia wamekuwa wakipewa mapumziko katika baadhi ya michezo ya ligi ili kujiandaa kwa hatua muhimu za Ligi ya Mabingwa.
Kutokana na hilo, PSG itaingia katika fainali hiyo ikiwa imepata siku 13 za mapumziko tangu mchezo wao wa mwisho wa ligi, wakati Arsenal watakuwa na siku sita pekee za kupumzika.
Arsenal ambao walitwaa ubingwa wa England msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22, wamekuwa na ratiba ngumu kutokana na ushindani mkubwa wa Ligi Kuu England.
Wachezaji muhimu wa timu hiyo akiwemo David Raya, Declan Rice, William Saliba na Martin Zubimendi wamecheza mechi nyingi zaidi za ligi msimu huu ukilinganisha na nyota wengi wa PSG.
Hata hivyo, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, anaamini kikosi chake kiko tayari kwa pambano hilo kubwa huku akitarajia kuiongoza klabu hiyo kutwaa taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
PSG nao wanataka kuendeleza ubabe wao Ulaya baada ya mafanikio ya misimu ya karibuni chini ya uwekezaji mkubwa wa Qatar Sports Investments.
Fainali hiyo inatarajiwa kuwa moja ya michezo mikubwa zaidi msimu huu huku timu zote mbili zikiwania kuandika historia mpya katika soka la Ulaya.




