Ligi Kuu

Prisons: Hatuwaogopi Azam tunawaheshimu

MBEYA: KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC huku akisisitiza kuwa wanawaheshimu wapinzani wao lakini hawataingia uwanjani kwa hofu.

Akizungumza jijini Mbeya kuelekea katika mchezo huo utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Sokoine, Nsajigwa amesema Azam ni timu yenye uzoefu na ubora mkubwa, hasa baada ya kushiriki mashindano ya kimataifa, jambo linalowapa makali ya ziada.

“Tunawaheshimu Azam FC na tunaamini tutakuwa na mechi nzuri. Ni timu yenye wachezaji wa daraja la juu na uzoefu mkubwa, lakini nasi tumejiandaa vizuri na tunaamini tuna uwezo wa kupata alama tatu,” amesema Nsajigwa.

Kocha huyo ameongeza kuwa maandalizi ya kikosi chake yamekuwa mazuri, akieleza kuwa wachezaji wake wako katika hali nzuri kimwili na kiakili kuelekea mchezo huo muhimu wa Ligi Kuu.

Kwa upande wake, mchezaji wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula, amesema jukumu kubwa sasa lipo mikononi mwa wachezaji kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya benchi la ufundi.

“Tumejiandaa vizuri na tunahitaji ushindi. Walimu wamemaliza kazi yao ya kutupa maelekezo, kilichobaki ni sisi kuingia uwanjani na kupambana ili tuondoke na alama tatu muhimu,” amesema Mbangula.

Related Articles

Back to top button