Onana kurejea kazini kesho

MANCHESTER, Meneja wa Manchester United Ruben Amorim amesema golikipa namba moja wa klabu hiyo Mcameroon Andre Onana atakuwa katika milingoti mitatu klabu hiyo itakapoivaa Lyon kwenye mchezo wa Europa league kesho Alhamisi.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo Amorim amethibitisha urejeo wa Onana ambaye alilaumiwa katika mchezo wa awali kwa klabu hiyo kukosa ushindi kutokana na makosa yake.
“Onana atacheza kesho, mimi kama kocha na mchezaji wa zamani kabla ya yote ni lazima nifanye mambo ya kumsaidia mchezaji katika hali zote, hapa nazungumzia kuhusu ‘kuwamanage’ wachezaji kimwili na kihisia”
“Imepita wikiendi ambayo niliona ni bora Onana apumzike na badala yake nikampa nafasi Altay (Bayandir) acheze” amesema Amorim
United wako nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi kuu ya England zikiwa zimesalia mechi 6 pekee msimu kumalizika. Ikiwa watamaliza katika nafasi hiyo itakuwa ndiyo nafasi ya chini zaidi kumaliza msimu tangu msimu wa 1973/74.
Amorim bado ana nafasi ya kuziba midomo na kuzima kelele za mashabiki wa timu hiyo ikiwa atamaliza msimu na kombe la Europa league ambalo ndio faraja pekee ya mashabiki hao wenye njonjo na hisia za aina yake na ni njia pekee ya kuthibitisha ujenzi wa kikosi hicho.