DAR ES SALAAM:MWIMBAJI nyota Peter Msechu amesema tangu alipofanyiwa upasuaji wa Gastric bypass ili kusaidia tatizo lake la uzito ameshapunguza kilo 27 hadi sasa.
Katika mtandao wa Twitter(X) Msechu alieleza kwamba tabia yake ya ulaji kupita kiasi ndiyo iliyomsababishia matatizo yake ya kuongezeka uzito jambo linalomsumbua kwa muda mrefu.
Msechu alisema kuna wakati aliongezeka uzito hadi alifika kilo zaidi ya 150.
“Nilipokuwa mdogo nilikuwa nikiwaambia wazazi wangu kwamba nitanunua magunia yangu ya mchele ili nile ninavyotaka. Nilikuwa nikiona hili ni jambo la thamani sana lakini kwa muda mrefu, hili lilinifanya niongezeke uzito,” alisema.
Msechu alieleza zaidi kuwa alikuwa akila sahani tatu za Wali na Chips katika mlo mmoja. Pia anasema alipenda vitu vya sukari.
“Ilifikia hatua nilipoona watoto wangu wakipewa chakula kizuri nilitaka pia chakula hicho, mwishowe, hii ilinipa wakati mgumu kiafya.
Januari 27. 2023 Msechu alikuwa miongoni mwa wagonjwa wanene waliowekewa puto ndani ya tumbo ili kuwasaidia kupunguza uzito.
Katika mchakato huo, alipoteza kilo 30. Hata hivyo, baada ya puto kuondolewa alipata uzito zaidi.
Upasuaji wa njia ya utumbo ili kuokoa maisha ya watu wengi hata wale walio na hali ya unene uliokithiri umefanyika kwa mafanikio kwa miaka mingi huku Willis Raburu, Big Ted, na Wema Sepetu wakiwa miongoni mwa mastaa waliowahi kufanyiwa upasuaji huo.