Mfaume atamba kummaliza Mnamibia

DAR ES SALAAM: BONDIA Mfaume Mfaume amesema hamuhofii mpinzani wake bondia Amavila Paulus wa Namibia kwani amejipanga kumkabili katika pambano litakalofanyika Desemba 26, mwaka huu Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili Mfaume alisema amefanya mazoezi ya kutosha nchini Afrika Kusini na kujifunza mbinu mpya hivyo anaamini uwezo wa kumpiga Paulus anao.
Alisema jambo la muhimu ni mashabiki kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo kumuunga mkono na yeye amejipanga kutowaangusha.
“Mimi na familia yangu ya Nàccoz tuko imara, tumejipanga vizuri kwa maandalizi ya muda mrefu yaliyofanyika Afrika Kusini katika kuhakikisha tunafanya vizuri dhidi ya wapinzani, niwaambie huyo Mnamibia lazima akae,”alisema.
Mfaume ni miongoni mwa mabondia watakaocheza mapambano ya utangulizi yasiyokuwa na mikanda kwa ajili ya kumsindikiza Yohana Mchanja atakayecheza na bondia wa Ufilipino katika kuwania mkanda wa WBO.
Rekodi za mtandao wa ngumi za box rec zinaonesha Mfaume amecheza jumla ya mapambano 26 ya kulipwa na kati ya hayo ameshinda 18, amepoteza nane na kupata sare mbili huku mpinzani wake akicheza mapambano 13 na kati ya hayo ameshinda 10, amepoteza mawili na sare moja.