Nyumbani

Ndumbaro awaita Wabrazil Tanzania

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro amewaomba wadau wa michezo kutoka Brazil kufungua ofisi nchini Tanzania ambayo itasaidia kutoa huduma ya michezo, ujuzi, utaalamu na Mawazo ya kuviendeleza vipaji kwa ukaribu zaidi.

Ndumbaro amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na wadau wa michezo kutoka nchini Brazil waliokuja Tanzania kwa lengo la kuzungumza na wadau wa sekta ya michezo ikiwemo Serikali na vyama vya michezo kuhusu ushirikiano katika sekta hiyo hususani mpira wa miguu na riadha.

Amesema Brazil wamepiga hatua sana katika michezo, ujio wao na kushirikiana nao kwa ajili ya kutaka kuona Tanzania inapiga hatua katika sekta hiyo kama ilivyo kwenye Taifa hili na kuwashauri wafungue ofisi nchini ili kuweza kutoa huduma za kimichezo kwa karibu zaidi.

“Tunamshukuru Balozi wa Tanzania nchini Brazil Prof. Adelardus Lubango Kilangi kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaleta wadau hawa wakubwa wa maendeleo ya michezo hapa nchini. hawa ndio aina ya Mabalozi ambao Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawataka wawepo na wafanye kazi kama hizi” amesema Ndumbaro.

Naye Balozi Kilangi ameishukuru Serikali kupitia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mapokezi mazuri akieleza kuwa mazungumzo yaliyofanyika kati ya Serikali na wadau hao wa sekta ya michezo nchini Brazil yatazaa matunda.

Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania, (TFF) Wallace Karia, amemshukuru Balozi na Serikali kwa ugeni huo wenye tija kwa maendeleo ya michezo nchini wakiahidi kutoa ushirikiano katika vikao vitakavyofanyika kabla kurejea Brazil.

Related Articles

Back to top button