Mwalimu aawapa zawadi marafiki zake

MOROGORO: MSHAMBULIAJI wa Simba, Seleman Mwalimu, amesema bao alilofunga katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar jana amelitoa kama zawadi maalumu kwa rafiki zake wa karibu Wilson Nangu pamoja na Montero ambao walimpa hamasa kubwa kabla ya mchezo.
Seleman alisema Nangu ni mmoja wa watu wake wa karibu ambaye pia ni shabiki mkubwa wa Simba na kwa sasa anapitia kipindi kigumu baada ya kupata majeraha.
“Nangu ni mtu wangu wa karibu sana, tunatoka mkoa mmoja. Kila mara kabla ya mechi huwa ananipa hamasa kubwa na kuniambia nijitahidi kufunga bao. Jana (juzi) usiku kabla ya mchezo alinipigia simu pamoja na Montero wakaniambia nihakikishe nafunga kwa ajili yao,” amesema.
Mshambuliaji huyo amesema pia amekuwa akipata sapoti kutoka kwa marafiki zake wengine ambao wamekuwa wakimtia moyo katika maisha na soka.
“Waliniambia nikifunga bao niwe nimelitoa kwao. Alhamdulillah nimefanikiwa kufunga na bao hili ni zawadi yao,” amesema.
Seleman aliongeza kuwa mbali na marafiki zake hao, bao hilo pia amelitoa kwa familia yake ambayo imekuwa ikimuunga mkono katika safari yake ya soka.




