Masumbwi

Mwakinyo aomba radhi baada ya kupoteza pambano

ABIDJAN: BONDIA nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo, ameomba radhi kwa mashabiki wake baada ya kupoteza pambano dhidi ya bondia wa Ufaransa, Michel Soro, katika pambano lililofanyika jijini Abidjan, Ivory Coast.

Kupitia ujumbe wake baada ya pambano hilo, Mwakinyo amesema anafahamu maumivu na masikitiko waliyonayo mashabiki wake kutokana na matokeo hayo, huku akisisitiza kuwa hatetei kushindwa kwake.

“Ninapenda nitoe pole za maumivu kwa wote mlioathirika au kushindwa kuelewa kilichotokea jana. Siyatetee matokeo ya kupoteza kwangu na sitafuti sababu, kwani huu ni mchezo na matokeo ni sehemu yake,” amesema Mwakinyo.

Bondia huyo alieleza kuwa kilichomuumiza zaidi si kupoteza pambano hilo, bali kushindwa kuonesha kiwango chake halisi kutokana na hali ya udhaifu aliyokuwa nayo wakati wa pambano.

Mwakinyo amesema alipambana na changamoto ya kuwa dhaifu na mwepesi kupita kawaida, jambo lililomzuia kujitetea na kupigana kwa mtindo ambao mashabiki wake wameuzoea kwa miaka mingi.

Alifafanua kuwa pambano hilo lilikuwa gumu na alijiandaa kwa nguvu zote katika mazoezi, lakini hali yake ya mwili siku ya pambano haikuwa katika kiwango bora cha kumwezesha kuonesha uwezo wake kamili.

“Haukuwa upiganaji ule ambao mmeuzoea. Ilikuwa ni mchezo mgumu ambao niliwekeza nguvu kubwa kwenye maandalizi, lakini niliingia ulingoni nikiwa dhaifu sana,” amesema.

Licha ya matokeo hayo, Mwakinyo amesema ameyapokea kwa moyo wa mchezo na kuahidi kurejea akiwa imara zaidi katika mapambano yajayo.

Related Articles

Back to top button