Mwagala ajivunia “TRA Effect”
ARUSHA: MSEMAJI wa TRA, Christina Mwagala, amesema hakuna timu yenye uwezo wa kuifunga TRA wanapocheza nyumbani Arusha kufuatia sare tasa waliyoipata dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana.
Mwagala amesema matokeo hayo yanaonesha uimara wa kikosi chao, akisisitiza kuwa walijiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo licha ya kulenga kupata ushindi.
“Simba hana timu ya kuifunga TRA na ndio kitu kimetokea. Sisi tulikuwa tunataka pointi tatu lakini tumepata moja, tunashukuru kwa hilo,” Amesema.
Ameongeza kuwa sare hiyo ni sehemu ya kile alichokiita “TRA effect”, akidai kuwa hakuna timu itakayokuja Arusha na kuondoka na ushindi kirahisi.
“Nawapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya. Hii ndiyo TRA effect maana yake hakuna timu itakayokuja hapa na kupata ushindi,” Amesisitiza.
Kwa matokeo hayo, TRA inaendelea kujiimarisha nyumbani huku ikipeleka ujumbe kwa wapinzani wake kuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid si sehemu rahisi kwa wageni kupata alama tatu.
Mwisho




