Muigizaji India alivyohofia kuuawa na walinzi wake

MUMBAI: MUIGIZAJI na muandaaji wa filamu nchini India, Rakesh Roshan amekumbuka namna alivyohofia kuuawa na walinzi wake baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye gari lake katikati ya barabara huko Mumbai nchini India.
Rakesh amesema baada ya tukio hilo ambalo hatolisahau lililomtokea mwaka 2000 alilazimika kuendesha gari hadi kituo cha polisi huku akiwa bado anavuja damu na baadaye akakimbizwa hospitalini.
Katika mahojiano na ANI nchini India, Rakesh amesema baada ya tukio hilo alipewa walinzi wawili wenye silaha, wengi walidhani atakuwa salama lakini kwake uwepo wa walinzi hao wanaume wawili ulizidi kumpa hofu zaidi kwani ‘aliogopa’ kwamba ingekuwa rahisi kwao kumuua.
Rakesh ameendelea kueleza kwamba:, “Haijalishi ni kiasi gani cha wafanyikazi wa usalama wapo karibu nami, ikiwa mtu anataka kukudhuru, wafanyikazi wa usalama hawataweza kufanya chochote.
“Nilichokuwa nikihofia ni kwamba nilikuwa nakaa mbele ya gari na wao wanakaa nyuma na bunduki, ikitokea kitu wanaweza kuniua, kwani kila sehemu hata sehemu za fukwe za starehe binafsi walikuwepo karibu yangu sikuwa na furaha hata kidogo zaidia ya kujawa hofu muda wote niliokuwa nao walinzi hao.”
Katika mazungumzo ya awali ya Zoom, Rakesh Roshan alisema kwamba alikuwa na dereva wake wakati risasi zilipofyatuliwa na dereva wake huyo alitetemeka kwa hofu mno. “Nilimwomba avute pumzi. Hadi wakati huo, sikutambua hata nilipigwa risasi. Kisha tukaelekea kituo cha polisi kwa sababu nilishuku kuwa wapigaji risasi wanaweza kuwa karibu, na wanaweza kukamatwa,” alikumbuka.