Filamu

Muigizaji India afariki dunia

INDIA: MUIGIZAJI wa India aliyetamba na filamu ya ‘Taj Mahal’, Manoj Bharathiraja amefariki dunia kwa mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 48.

Filamu nyingine alizocheza muigizaji huyo ni ‘Samudhiram’ na ‘Alli Arjuna’, na amefariki akiwa huko Chennai nchini India.

Meneja wa muigizaji huyo amethibitisha habari za kifo hicho kwa News18. Manoj, amesema muigizaji huyo alifanyiwa upasuaji hivi karibuni na alipata nafuu alipokuwa nyumbani kwake Chetpet hadi jana jioni alipopatwa na mshtuko wa moyo.

Meneja huyo amesema, “Manoj alifanyiwa upasuaji hivi karibuni na alikuwa akiendelea kupata nafuu. Hata hivyo, alipatwa na mshtuko wa moyo akiwa nyumbani kwake, jambo lililowashtua watu wote. Mazishi na mambo mengine bado hayajaamuliwa.” Ameeleza.

Manoj ameacha mke, Ashwathi almaarufu Nandana, na mabinti wawili, Arshitha na Mathivathani. Alionekana mara ya mwisho katika mfululizo wa mtandao wa ‘Snakes & Ladders Tamil’, ambao ulitolewa mwaka wa 2024.

Watu mashuhuri wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuomboleza msiba huo akiwemo Khushbu Sundar aliyeandika katika mtandao X, “Nimeshtushwa sana kusikia kwamba Manoj hayuko miongoni mwetu tena. Maumivu yake ya kifo cha ghafla. Alikuwa na umri wa miaka 48 tu. Mungu ampe nguvu baba yake na familia yake washinde msiba huu mchungu usiovumilika. Utamkosa Manoj. Pumzika kwa amani. Om Shanthi.”

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button