Ligi Daraja La Kwanza

Mtibwa, Geita ni mwendokasi mpaka Ligi Kuu

DAR ES SALAAM: Timu za mtibwa Sugar na Geita Gold hazikamatiki kunako ligi ya Championship zikiongoza kwa kufanya vizuri mpaka sasa.

Kinara huyo wa Manungu katika michezo 12, ameshinda michezo tisa, amepata sare mbili na kupoteza mmoja akiwa na pointi 29 huku Geita akishinda michezo nane, akipoteza mmoja na kupata sare tatu akiwa na pointi 27.

Kwa mwenendo wa timu hizo kama wataendelea hivyo, wanaweza kurejea Ligi Kuu msimu ujao.

Msemaji wa Mtibwa Thobias Kifaru amekuwa na jeuri ya kusema kuwa kulingana na ubora wa kikosi wana nafasi ya kurejea Ligi Kuu msimu ujao.

“Hakuna wa kutuzuia, sababu tuna kikosi kizuri na mwalimu mzuri na tunashinda mechi. Naimani tutarejea tukiwa imara zaidi,”amesema.

Msemaji wa Geita Samwel Dida amesema malengo yao ni kurejea Ligi Kuu ndio maana kila mechi kwao wanachukulia kama fainali na kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu.

Ingawa bado kuna upinzani kwa timu kama Stand United iliyoko katika nafasi ya tatu kwa pointi 23 ikifuatiwa na Mbeya City katika nafasi ya nne kwa pointi 22.

Safari ni ndefu ya kumaliza mzunguko wa kwanza kisha mzunguko wa pili ambao utaamua hatma ya nani atapanda, nani kucheza hatua ya mtoano na nani kubaki alipo.

Related Articles

Back to top button