Kwingineko

Mitaa ya Cape Verde yaendeleza furaha, Golikipa Vozinha atajwa kila kona

CAPE VERDE: KATIKA Jiji la Praia na maeneo mengine nchini Cape Verde, wananchi walisherehekea matokeo ya sare ya 0-0 dhidi ya mabingwa wa zamani wa Kombe la Dunia Hispania, wenye magari walipiga honi, wengine walipeperusha bendera za taifa na kuimba nyimbo za kuisifu timu yao.

Pia mitandao ya kijamii nchini humo ilifurika jumbe za pongezi kwa kikosi hicho, huku jina la Vozinha likitajwa mara kwa mara kama alama ya matumaini na uzalendo kwa nchi yake.

Kilichovutia zaidi ni namna ulimwengu wa soka ulivyompongeza Vozinha. Wachezaji wa zamani, wachambuzi na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali walitumia mitandao ya kijamii kumwelezea kama ‘ukuta usiovunjika’ na ‘shujaa wa kweli wa Kombe la Dunia’. Katika kipindi cha saa chache baada ya mechi kumalizika, picha na video za save zake zilikuwa zikisambazwa kwa maelfu ya watu duniani.

Wachambuzi wa soka nchini humo wameeleza kuwa matokeo hayo yana thamani kubwa kuliko pointi moja waliyoipata. Kwao, sare dhidi ya Hispania ni uthibitisho kwamba Cape Verde sasa inaweza kushindana na mataifa makubwa ya soka duniani. Wengi wameeleza kuwa timu hiyo imeonesha nidhamu, moyo wa kujituma na umoja ambao mara nyingi huonekana katika timu zinazofika mbali kwenye mashindano makubwa.

Taifa hilo dogo la visiwa vya Afrika Magharibi, lenye idadi ya watu wasiopungua milioni moja, limefanikiwa kusimama imara mbele ya moja ya timu zenye vipaji vikubwa zaidi duniani na kuwafanya mashabiki wao kuamini kuwa ndoto ya kufanya makubwa katika Kombe la Dunia inaweza kutimia.

Shujaa golikipa mkongwe Vozinha alifanya mfululizo wa save za kiwango cha juu na kuzuia mashambulizi ya Hispania yaliyokuwa yakiongozwa na nyota wao mbalimbali. Kila shambulizi lililoelekezwa golini lilimkuta Vozinha akiwa tayari kuokoa jahazi la timu yake, jambo lililomfanya kuwa gumzo duniani kote mara baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa.

Kocha wa Cape Verde pia alisifiwa kwa mbinu zake za kujihami na namna alivyofanikiwa kuzuia mashambulizi ya Wahispania kwa dakika zote 90. Wachezaji wa safu ya ulinzi walifanya kazi kubwa ya kumlinda golikipa wao huku wakionesha utulivu wa hali ya juu licha ya kukabiliwa na presha kubwa kutoka kwa wapinzani wao.

Kwa upande wa Hispania, matokeo hayo yalionekana kama pigo kwa matarajio yao ya kuanza mashindano kwa ushindi. Mashabiki wengi wa Hispania walionesha kusikitishwa na kushindwa kwa timu yao kutumia nafasi nyingi walizotengeneza, huku wakikiri kwamba Cape Verde ilistahili pointi hiyo kutokana na kiwango kikubwa ilichoonesha.

Kwa sasa, matumaini ya Cape Verde yameongezeka maradufu kuelekea mechi zijazo za Kundi H. Mashabiki wanaamini kuwa kama timu yao inaweza kuizuia Hispania, basi inaweza pia kupambana na timu nyingine katika kundi hilo na kuandika historia zaidi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button