Mitindo

Miriam Odemba: “Mimi ni legendary Queen, historia yangu haiwezi kufutwa”

DAR ES SALAAM:MREMBO na mwanamitindo wa kimataifa, Miriam Odemba, amefunguka na kutoa ufafanuzi kuhusu historia ya mashindano ya urembo, akiwataka Watanzania kuelewa tofauti za mashindano hayo na kuheshimu mafanikio ya kila mshiriki.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Odemba amesema “ulimwengu wa mashindano ya urembo (pageantry) una historia, hadhi na mifumo tofauti ya ushindani ambayo inapaswa kueleweka kabla ya kuwalinganisha warembo.

Odemba ameeleza kuwa aliporejea Tanzania, alipokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi, akisema mapokezi hayo yalikuwa ya kihistoria kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kumpokea katika uwanja wa ndege.

Amesema tukio hilo” lilimpa nipa nafasi ya kuona upendo mkubwa aliopokea kutoka kwa Watanzania, jambo ambalo analithamini na kulipokea kwa moyo wa shukrani.”

Akizungumzia historia yake katika mashindano ya urembo, Odemba amesisitiza kuwa safari yake ya kimataifa imejengwa kwa miaka mingi kupitia mashindano mbalimbali na mataji aliyopata.

Miongoni mwa mafanikio aliyoyataja ni kuwa Face of Africa 1999, mshindi wa Elite Model Look na Miss Earth Air 2008, pamoja na kutaja mashindano mengine ya urembo ambayo amewahi kushiriki.

Aidha, Odemba amezungumzia mafanikio ya Jihan, akimpongeza kwa ushindi wake na kumtakia mafanikio katika safari yake ya kimataifa. Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio ya Jihan hayapaswi kutumika kufuta au kupunguza historia ambayo yeye ameijenga kwa muda mrefu.

“Mimi nina historia yangu, na Jihan ana safari yake. Hatuhitaji kumshusha mmoja ili kumuinua mwingine,” ameandika Odemba.

Ameongeza kuwa si sahihi kuwalinganisha warembo kwa kuangalia nafasi walizofikia katika mashindano, kama vile Top 40, Top 20, Top 10 au Top 6, bila kuzingatia aina ya mashindano, historia yake na mfumo wa ushindani unaotumika.

Kwa mujibu wa Odemba, kila mashindano yana sifa na vigezo vyake, hivyo ni muhimu kwa mashabiki wa urembo kufanya utafiti na kuelewa tofauti zilizopo kabla ya kutoa maoni au kufanya ulinganisho.

Akijitambulisha kwa kujiamini, Odemba amesema uzoefu wake wa zaidi ya miaka 30 katika ulimwengu wa urembo umemjengea jina ambalo, kwa mtazamo wake, linazidi ushindi wa shindano moja.

“Mimi ni Miriam Odemba. Mimi ni Legendary Queen. Mimi ni Mama wa Urembo. Historia yangu haiwezi kufutwa na mafanikio ya mtu mwingine,” amesema.

Pamoja na msimamo huo, Odemba amesisitiza kuwa anawaheshimu warembo wote na anaunga mkono mafanikio ya wanawake wenzake, huku akitamani kuona Tanzania ikiendelea kung’ara katika mashindano ya urembo ya kimataifa.

Amehitimisha kwa kuwataka Watanzania kujifunza zaidi kuhusu mashindano kama Miss Earth na Miss Grand International ili waweze kushiriki mijadala ya urembo kwa kutumia maarifa, heshima na hoja zenye msingi.

Kauli yake imeweka msisitizo katika umuhimu wa kutambua mafanikio ya warembo wapya bila kusahau mchango na historia ya wale waliotangulia katika tasnia hiyo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button