Familia

Lulu atoa ya moyoni kuhusu malezi ya watoto katika Dunia ya sasa

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini Tanzania, Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu, amefunguka kuhusu wasiwasi alionao juu ya malezi ya watoto wake katika dunia ya sasa, akieleza kuwa mazingira ya maisha yamebadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Lulu amesema dunia ya sasa ina tofauti kubwa na ile waliyoizoea watu wa kizazi chake, huku maendeleo ya teknolojia na matumizi ya mitandao ya kijamii yakiendelea kubadilisha namna watu wanavyoishi, wanavyowasiliana na wanavyovichukulia mambo mbalimbali.

Akieleza kuhusu jambo hilo, msanii huyo amesema moja ya changamoto zinazompa mawazo ni namna watoto wake watakavyokabiliana na mazingira ya dunia wanayokulia, ambayo anaona yanazidi kubadilika kadiri siku zinavyosonga.

“Wasiwasi wangu mkubwa kwa wanangu ni jinsi walivyoikuta dunia. Miaka ambayo tumezaliwa sisi na ukiangalia kwa sasa hivi ni tofauti, kadri siku zinavyozidi kwenda dunia inazidi kuwa ya aina yake,” amesema Lulu.

Aidha, Lulu amebainisha kuwa mitandao ya kijamii imechukua nafasi kubwa katika maisha ya kila siku, hali inayofanya malezi ya watoto katika kipindi hiki kuhitaji umakini zaidi kutoka kwa wazazi.

Amesema kutokana na hali hiyo, amekuwa akijitahidi kuwafundisha watoto wake kuwa wakakamavu ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha, huku akiendelea kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu.

“Ninachokifanya kila siku huwa nawafundisha watoto wangu wawe wakakamavu huku nikizidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu,” amesisitiza Lulu.

Kauli ya Lulu inaibua mjadala kuhusu nafasi ya wazazi katika kuwalea watoto katika zama ambazo teknolojia, mitandao ya kijamii na mabadiliko ya kijamii vinaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.

Je, unadhani wazazi wa sasa wanapaswa kufanya nini ili kuwalinda na kuwaandaa watoto wao kukabiliana na changamoto za dunia ya leo?

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button