Nyumbani

Simba yataka Uhuru ujazwe

Doumbia mgeni rasmi

DAR ES SALAAM:KLABU ya Simba imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC 15 de Agosto ya Equatorial Guinea, itakayochezwa Jumapili Oktoba 25, 2026, saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mchezo huo ni fursa kwa mashabiki kuishukuru na kuipongeza timu yao kwa kazi iliyofanya hadi kufikia hatua ya kukaribia kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Ahmed amesema licha ya Simba kuwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, mashabiki hawapaswi kuuchukulia mchezo huo kuwa hauna umuhimu, bali wajitokeze uwanjani kuipa timu hamasa na kuadhimisha mafanikio yake.

“Rai yangu kwa mashabiki wa Simba ni Oktoba 25 isibaki siti hata moja. Heshima kwa wachezaji wetu siyo kupost mitandaoni, bali ni kwenda uwanjani kuwapongeza kwa kazi kubwa ambayo wameifanya,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa klabu hiyo inataka kutumia mchezo huo kuweka rekodi nzuri ya mabao katika hatua za kufuzu, akieleza kuwa Simba imefunga mabao sita hadi sasa, huku akitaka timu hiyo iendelee kuongeza idadi hiyo inapopata nafasi.

Katika hatua nyingine, Ahmed ametangaza kuwa kiungo mshambuliaji Ibrahim Doumbia atakuwa mgeni rasmi wa mchezo huo, akisema uamuzi huo umetokana na safari aliyopitia ndani ya klabu hiyo pamoja na mchango wake katika mchezo uliopita, ambako alifunga mabao mawili.

Amesema Doumbia amepitia changamoto na maneno mbalimbali, lakini baadhi ya mashabiki waliendelea kumuunga mkono hadi alipoanza kuonesha uwezo wake uwanjani hasa katika mchezo uliopita baada ya kufunga mabao mawili.

Related Articles

Back to top button