Nyumbani

Guinness yaileta kombe la Ligi Kuu ya England Tanzania

DAR ES SALAAM: Soka si dakika 90 pekee uwanjani. Ni mijadala isiyoisha hata baada ya filimbi ya mwisho, jezi zinazovaliwa kwa fahari, mitaa yenye mashabiki wanaoshikilia timu zao kwa dhati na urafiki unaodumu licha ya ushindani mkali wa timu pinzani. Hivyo, Kombe la Ligi Kuu ya England lilipotua Tanzania, liliwasili katika jiji ambalo halihitaji kufundishwa maana ya kuipenda soka.

Kwa siku mbili, kombe hilo likawa kitovu cha shauku hiyo. Kupitia Guinness, Mdhamini Rasmi wa Bia wa Ligi Kuu ya England, kombe hilo lilitembelea Tanzania kwa mara ya kwanza, likiwavuta mashabiki mitaani na baadaye kuwakutanisha katika hafla kubwa ya soka iliyounganisha mapenzi ya Ligi Kuu ya England na ushindani mkali wa soka la nyumbani.

Kupitia kampeni ya Guinness ya “Tanzania Goes EXTRA”, ziara hiyo haikuwa tu kuhusu kuleta kombe maarufu nchini. Ilikuwa ni kulitoa soka kwenye runinga na kulipeleka karibu na mashabiki, kwenye mitaa, mazungumzo na jamii ambazo zinaendelea kuishi na soka hata baada ya mechi kumalizika.

JIJI LA DAR ES SALAAM LIKAPOKEA NDOO

Safari ya kombe hilo ilianza Oktoba 9, 2026, lilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Kuanzia hapo, Dar es Salaam ikawa sehemu ya shamrashamra za mapokezi yake.

Msafara ulianzia Uwanja wa Uhuru na kupita Chang’ombe, Mbagala, Temeke, Tazara, Buguruni, Kariakoo, Magomeni na Kinondoni, kabla ya kuhitimishwa Coco Beach. Katika maeneo hayo tisa yaliyotajwa, mashabiki walijitokeza kando ya njia ya msafara wakisubiri kuliona kwa karibu kombe ambalo kwa mamilioni ya watu duniani ni alama ya mafanikio makubwa katika soka la klabu nchini England.

Uzito wa ziara hiyo haukuwa kwenye kombe lenyewe pekee, bali pia kwenye safari yake katikati ya jiji. Badala ya kubaki kwenye hafla ya watu wachache, kombe hilo lilipita kwenye maeneo ambayo soka ni sehemu ya maisha ya kila siku,maeneo ambako mashabiki hujadili timu zao, hutetea chaguo zao na kurithisha mapenzi ya soka kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kwa waliotoka kulishuhudia, ilikuwa nafasi adimu ya kukutana ana kwa ana na alama inayowakilisha mashindano wanayofuatilia kila wiki.

Safari hiyo pia ilihusisha ziara katika Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania kwa ajili ya shughuli za ushirikishwaji wa wadau. Baadaye jioni, shamrashamra ziliendelea katika ukumbi wa The Superdome, ambako wageni waalikwa, wadau, na vilabu mbalimbali vya mashabiki wa timu za ligi kuu ya England walishiriki hafla maalumu ya kuliona kombe hilo. Kulikuwa pia na uzoefu maalumu kwa mashabiki wakereketwa wa soka, ukiwatambua wafuasi ambao mapenzi yao kwa mchezo huo yanaifanya soka kuwa zaidi ya burudani ya siku ya mechi.

Kwa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), ziara hiyo ilidhihirisha nafasi ya kipekee ambayo soka inayo katika maisha ya Watanzania na namna uzoefu kama huo unavyoweza kuwaleta mashabiki karibu zaidi na mchezo wanaoupenda.

“Soka nchini Tanzania si mchezo tu, bali ni shauku inayowaunganisha mamilioni ya watu. Tunajivunia kuona Guinness ikileta Kombe la Ligi Kuu ya England nchini kwa mara ya kwanza, na kuwapa mashabiki nafasi ya kuukaribia zaidi mchezo wanaoupenda,”alisema Dk. Obinna Anyalebechi, Mkurugenzi Mkuu wa SBL.

KISHA IKAFIKA ZAMU YA DABI YA KARIAKOO

Ikiwa msafara ulipeleka kombe karibu na mashabiki mitaani, siku iliyofuata, Oktoba 10, Guinness Matchday katika Uwanja wa KMC, Mwenge, iliwakusanya mashabiki hao katika eneo moja kwa ajili ya kushiriki burudani ya soka.

Jumla ya mashabiki 2,500 walikusanyika kushuhudia mechi za Ligi Kuu ya England, zikiwemo Arsenal dhidi ya Leeds United na Manchester United dhidi ya Tottenham Hotspur. Kwa mashabiki waliozoea kufuatilia timu zao kupitia runinga, ilikuwa nafasi ya kufurahia mechi pamoja na wapenzi wengine wa mchezo huo.

Lakini tukio lililoipa siku hiyo ladha halisi ya Kitanzania lilikuwa Dabi ya Kariakoo.

Mechi ya Simba SC dhidi ya Young Africans SC nayo ilionyeshwa mubashara katika Uwanja wa KMC, sambamba na mechi za Ligi Kuu ya England. Hapo ndipo shamrashamra hizo zilipopata sura ya kipekee ya Kitanzania. Haikuwa tena habari ya kombe maarufu la soka la England pekee, bali pia ilikuwa kuhusu ushindani wa ndani unaovuta hisia za mashabiki kote nchini.

Hapo ndipo dunia mbili za soka zilipokutana: Ligi Kuu ya England, inayofuatiliwa kwa shauku na mashabiki wengi nchini, na dabi ya nyumbani ambayo rangi za timu, historia na ushindani wake vina mizizi mirefu katika jamii. Mashabiki walikutana katika uwanja mmoja kufuatilia mechi hizo, kila mmoja akiwa na timu yake moyoni, lakini wote wakiwa sehemu ya sherehe moja ya soka.

Hiyo ndiyo iliyokuwa nguvu halisi ya tukio hilo. Kombe lilikuwa kivutio kikuu, lakini mashabiki ndio waliolipa tukio hilo uhai. Katika Uwanja wa KMC, soka la kimataifa halikuchukua nafasi ya utamaduni wa soka la nyumbani; badala yake, mambo hayo mawili yalienda pamoja. Kuwepo kwa Dabi ya Kariakoo kulifanya sherehe hizo ziakisi uhalisia wa soka la Tanzania, badala ya kuonekana kama tukio lililoletwa kutoka nje pekee.

Kwa Geoffrey Lea, mmoja wa mashabiki waliohudhuria, kuliona kombe hilo Dar es Salaam kulifanya mapenzi yake ya kawaida kwa soka kuwa uzoefu wa kipekee.

“Tunafurahia kutazama Ligi Kuu ya England kila wiki, lakini kuliona kombe hilo hapa Dar es Salaam ilikuwa ni uzoefu wa kipekee kabisa. Ilikuwa furaha kubwa kuliona kwa karibu na kuwa sehemu ya tukio lililowakutanisha mashabiki wengi wa soka,”alisema.

Naye Joseph Machera, shabiki mwingine aliyehudhuria tukio hilo, alisema mchanganyiko wa mechi za Ligi Kuu ya England na Dabi ya Simba na Yanga ndio uliofanya siku hiyo kuwa ya kipekee.

“Tunafurahia kutazama Ligi Kuu ya England kila wiki, lakini kuliona kombe hilo hapa Dar es Salaam ilikuwa ni uzoefu wa kipekee kabisa. Ilikuwa furaha kubwa kuliona kwa karibu na kuwa sehemu ya tukio lililowakutanisha mashabiki wengi wa soka,”alisema.

Kwa Henry Esiaba, Mkurugenzi wa Ubunifu na Masoko wa SBL, mwitikio wa mashabiki ulidhihirisha shauku ya soka ambayo mtu anaielewa vizuri zaidi anapoishuhudia mwenyewe.

“Huwezi kuelewa kikamilifu namna Watanzania walivyo na shauku na soka mpaka ujionee mwenyewe. Guinness imeleta Kombe hili nchini ili kuwapa mashabiki nafasi ya kusherehekea mchezo wanaoupenda kwa namna ya kipekee,”alisema.

Ziara hiyo pia ilitambuliwa na viongozi wa soka na michezo nchini. Almasi Jumapili Kasongo, Mkurugenzi wa Timu za Taifa katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), alisema kuwasili kwa kombe hilo kulionesha uhusiano uliopo kati ya mashabiki wa Tanzania na soka la kimataifa.

Kwa upande wake, Neema Msita, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BST), alisisitiza nafasi ya michezo katika kuwaunganisha watu, kutengeneza fursa na kuonesha utamaduni pamoja na vipaji. Ushiriki wao uliongeza uzito wa tukio lililowakutanisha mashabiki, wadau na washirika kupitia mapenzi ya pamoja kwa soka.

Washirika wa kibiashara wa Guinness nao walishiriki katika kuunga mkono shamrashamra hizo, wakisaidia kuunganisha ziara ya kombe hilo na maeneo ambako mashabiki hukutana mara kwa mara kufuatilia mechi.

Ziara ya kombe hilo nchini ilipofikia tamati, ilikuwa imeacha simulizi iliyozidi mfululizo wa hafla na shughuli zilizopangwa. Safari yake ilianzia mitaani na kuishia kwenye mkusanyiko wa mashabiki waliokutana kushuhudia soka la kimataifa huku wakifuatilia pia ushindani mkali wa Dabi ya Kariakoo.

Kwa jiji ambalo soka ni sehemu ya mazungumzo ya kila siku, ziara hiyo iliwapa mashabiki nafasi nyingine ya kuusherehekea mchezo wanaoupenda kwa namna yao, mechi za timu kubwa za England zikioneshwa kwenye skrini, wapinzani wa nyumbani wakipambana uwanjani, na Kombe la Ligi Kuu ya England likiwa katikati ya tukio hilo.

Related Articles

Back to top button