Mipango timu ya taifa mpira wa wavu yasukwa

KATIBU wa Shirikisho la Mpira wa Wavu Tanzania (TVL), Lawrence Safari amesema wanatarajia kupata timu ya taifa bora kupitia mashindano ya taifa, yanayoendelea katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar es Salaam.
Amesema ushindani umekuwa mkubwa hali ambayo inawapa wakati mgumu kutambua mapema nani atachukuwa ubingwa wa mashindano hayo ya Taifa.
“Tunaimani hatua hii wataalamu wetu watapata timu nzuri ya Taifa kwa sababu ya ushindani unaoneshwa na wachezaji kila mmoja anaonesha ubora kwa timu yake.
“Malengo yetu yalikuwa kupata klabu 24 lakini 17 zimefanikiwa kushiriki, sababu kubwa ya hizo klabu zingine ni ukata wa kiuchumi na majukumu ya wachezaji ambao ni wafanyakazi na wanafunzi,” amesema Lawrence.
Ameeleza kuwa mashindano hayo yana mchango kubwa wa kutengeneza timu ya taifa, makocha wa timu za taifa wanaangalia wachezaji walioonesha ubora baadae wawaite katika kikosi.