“Mechi haijaisha” – Ancelotti

LONDON:Bosi wa Real Madrid Carlo Ancelotti amekiri kuwa kuna nafasi finyu ya kikosi chake kuvuka kigingi cha robo fainali na kwenda nusu fainali lakini ameonya kuwa mechi haijaisha na Madrid wanaweza kufanya maajabu wakiwa katika dimba lao la Santiago Bernabeu.
Mchezo wa jana wa Arsenal dhidi Real Madrid ulishuhudia magoli mawili ya maajabu ya Declan Rice kabla ya Mikel Merino kupigilia chuma cha tatu na kuongeza mlima wa kupanda katika mchezo wa mkondo wa pili kwa mabingwa hao mara 15 wa Ligi ya mabingwa.
Ukiacha kipigo hicho mashabiki wengi wa Real Madrid wana wasiwasi juu ya mwendo wa kuchechemea wa klabu hiyo timu ikionekana kuvurugika kwenye safu ya ushambulizi na ulinzi japo kwenye baadhi ya michezo wameshinda.
“Kwa kawaida timu hii inapata moto zaidi mwisho wa mchezo, ilinivunja moyo hatukucheza vizuri hata kidogo, tulipaswa kuwa katili, tumejifunza tujikosoe hapa na tukamalize mchezo nyumbani, mechi haijaisha” – Amesema
Real Madrid wana rekodi ya kutisha ya kupindua matokeo, hasa wakiwa nyumbani kwao Santiago Bernabeu, na sio ajabu likatokea tena watakapoikaribisha Arsenal wiki ijayo.