Mastaa wa muziki wakutana tuzo za Trace The Mora Zanzibar
ZANZIBAR: WASANII Diamond Platinumz wa Tanzania, Rema wa Nigeria na Fally Ipupa kutoka Congo ni miongoni mwa idadi kubwa ya wasanii wanaotarajiwa kutumbuiza leo katika usiku wa tuzo za Trace 2025 zitakazofanyika katika hoteli ya The Mora Zanzibar iliyopo Unguja Kaskazizi A, visiwani Zanzibar.
Fally Ipupa ambaye Msanii Bora wa Kiume aliyeshinda tuzo hizo kwa mwaka 2023 anatarajiwa kukonga nyoyo za wahudhuriaji wa tuzo hizo leo usiku akishiriki jukwaa moja na wasanii kutoka nchi mbalimbali wakiwemo Rema na Diamond.
Katika kuongeza mvuto wa tuzo hizo wasanii mbalimbali wameshawasili visiwani Zanzibar na wengine wameonekana wakifurahia madhari huku wakikatiza huku na kule na kufanya mazungumzo kama Zuchu na msanii kutoka Nigeria Yemi Alade wameonekana wakibadilishana Mawazo kuelekea usiku huo wa aina yake utakaofanyika Zanzibar.
Licha ya tuzo hizo Trace waliandaa mazungumzo mbalimbali yakiwemo “Wasanii wa Kiafrika wanawezaje kupata mapato halisi tangu mwanzo?”,
“Wanawake katika Muziki wa Kiafrika: Ndoto au Ukweli?” na mazungumzo muhimu kuhusu nafasi ya wanawake katika tasnia ya muziki barani Afrika ambapo msanii kutoka Angola Chelsea Dinorath, Seven Mosha, Meneja Maendeleo ya Msanii Afrika Mashariki katika Sony Music, Valerie Gilles-Alexia, Meneja Mradi wa Tuzo za Trace na wengine wengi walijadiliana katika mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Izilda de Brito Robalo.