Mastaa

Mashitaka ya ubakaji yapandisha mauzo ya muziki wa P.Diddy

NEW YORK: BAADA ya nyota wa muziki wa hip hop nchini Marekani Sean Combs maarufu P. Diddy kushitakiwa kwa biashara ya ngono na ulaghai, kukamatwa kwake na kufikishwa mahakamani wiki iliyopita, mauzo ya muziki wake katika mitandao mbalimbali imepanda ghafla.

Kampuni ya data na uchanganuzi ya Luminate ilisema muziki wa gwiji huyo wa hip-hop ulishuhudia ongezeko la wastani la 18.3% la namna ilivyopakuliwa mitandaoni kwa wiki ya kukamatwa kwake ikilinganishwa na wiki iliyopita.

Profesa wa Usimamizi wa Biashara ya Muziki katika Chuo cha Muziki cha Berklee, George Howard alisema hashangazwi na ongezeko hilo kwa kuwa wengi walikuwa wakimtafuta mtandaoni kutokana na taarifa za mashitaka yake.

“Muziki ni sehemu nyingine ya Habari, watu wanajaribu kuelewa kwa undani kinachoendelea kwake,” Howard aliiambia AP,”

Howard alisema licha ya Diddy kuingia ubia na kampuni kadhaa ikiwemo Revolt TV na Ciroc vodka, ambazo kwa sasa hausiki nazo lakini bado watu wengi wanamfikiria Diddy kama mfanyabiashara na mwanamuziki.

Kuongezeka kwa mauzo ya muziki wa Diddy pia kumefananaishwa na mauzo yalivyoongezeka kwenye muziki wa R.Kelly anayetumikia kifungo jela kwa sasa baada ya kukutwa na makosa ya kingono.

Combs anashtakiwa kwa biashara haramu ya ngono na ulaghai na hati ya mashtaka, ambayo inaelezea madai yaliyoanzia 2008, inamtuhumu kwa kuwadhulumu, kutishia na kulazimisha wanawake kutimiza tamaa zake za ngono, kulinda sifa yake na kuficha maovu yake, lakini amekana mashitaka hayo.

Related Articles

Back to top button