AFCON 2027 kuitangaza Tanzania duniani

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yatakuwa fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Amesema mashindano hayo yanayoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda yatatoa jukwaa kubwa la kuitambulisha Tanzania kwa mamilioni ya watu duniani, huku yakichochea ukuaji wa sekta ya utalii hata baada ya mashindano kumalizika.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Kijaji amesema Tanzania ina vivutio vingi vya kipekee, vikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Zanzibar na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Amesema pamoja na vivutio hivyo, nchi inapaswa kuendelea kuboresha huduma za utalii, kuongeza aina za uzoefu kwa wageni na kufikia masoko mapya ili kutumia vyema fursa zitakazotokana na mashindano hayo.
“AFCON 2027 haitaleta wageni kwa kipindi cha mashindano pekee, bali ni uwekezaji wa kimkakati katika utangazaji wa utalii ambao unaweza kuendelea kuzalisha mahitaji ya huduma za utalii hata baada ya mashindano kumalizika,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kuratibu maandalizi yanayohusisha huduma za afya, usafiri, usalama na utalii, huku ikishirikiana na wadau wa sekta hiyo kuhakikisha hoteli na maeneo ya malazi yanakuwa tayari kuwapokea wageni.
Ameongeza kuwa maandalizi hayo yanahusisha wadau wa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha wageni watakaofika nchini wanapata huduma bora na nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ndani ya Maandalizi ya AFCON 2027, Leodgar Tenga, amesema mashindano hayo hayatakuwa tukio la kawaida la kimichezo, bali tamasha kubwa litakaloiunganisha Afrika Mashariki.
Tenga amesema maandalizi ya mashindano hayo yanatoa nafasi kwa nchi mwenyeji kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wageni wanapata huduma na uzoefu utakaowafanya kutamani kurejea tena katika ukanda huo.
Amesema Tanzania inafurahi kuwa sehemu ya maandalizi hayo na iko tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha AFCON 2027 inakuwa tukio lenye mafanikio kwa ukanda wa Afrika Mashariki.




