Yanga: Wachezaji 30 wako fiti kuivaa MC Alger

ZANZIBAR: YANGA SC imesema wachezaji wake wote 30 waliosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria wako katika hali nzuri na hakuna aliyepata majeraha kuelekea pambano hilo la Jumamosi.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu hiyo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema morali ya wachezaji iko juu huku kikosi kikiendelea na mazoezi katika viwanja vya New Amaan Complex, Zanzibar, kikilenga kuanza hatua ya makundi kwa ushindi.
Amesema MC Alger tayari imewasili Zanzibar pamoja na baadhi ya mashabiki wake na kwa mujibu wa ratiba, timu hiyo itafanya mazoezi kwa siku mbili kabla ya mchezo huo.
“Wachezaji wote 30 waliosafiri kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar wako katika hali nzuri na tunamshukuru Mwenyezi Mungu, hatujapata majeraha yoyote. Tunaendelea na maandalizi yetu huku morali ikiwa juu,” amesema.
Ameongeza kuwa hali hiyo inampa kocha mkuu wa Yanga, Fadlu Davids, nafasi ya kuwa na machaguo mengi ya wachezaji watakaoweza kutumika katika mchezo huo muhimu.
Aidha, amewataka wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga kuwahi kununua tiketi zao mapema kupitia simu ili kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo.
Amesisitiza kuwa nguvu ya mashabiki itakuwa sehemu muhimu ya kuipa timu hamasa ya kupata matokeo mazuri na kuanza kampeni ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo.




