Man City yatinga 16 bora kibabe

ORLANDO, Wababe wa soka la England Manchester City wamejihakikishia nafasi ya kwanza kwenye Kundi G la Kombe la Dunia la Klabu baada ya kuichakaza vibaya Juventus mabao 5-2 usiku wa kuamkia leo na kufichua udhaifu wa safu ya ulinzi ya timu hiyo ya Serie A.
Huku timu zote zikiwa tayari zimefuzu kwa hatua ya 16 bora, Man City walionesha njaa ya taji hilo ikiwa ni timu pekee iliyomaliza hatua ya makundi kwa kushinda mechi zote tatu ikionesha kiwango cha hali ya juu na kumaliza pointi tatu mbele ya Juventus, ambao watakutana na Real Madrid katika hatua ya 16 bora.
City walichukua uongozi wa mapema kwa bao la Jeremy Doku kwa pasi nzuri kutoka kwa mchezaji mpya Rayan Ait-Nouri kabla ya Juventus kujibu haraka wakitumia makosa ya mlinda mlango wa City Ederson aliyeadhibiwa na Teun Koopmeiners.
Bao la pili la Man City lilipatikana dakika ya 26 baada ya Beki wa Juventus Pierre Kalulu kuuweka kimeani mpira wa krosi wa Matheus Nunes alipokuwa katika jitihada za kuokoa. Kabla ya timu hiyo ya Premier League kuongeza la tatu kutoka kwa Erling Haaland baada ya asisti nyingine ya Nunes.
Phil Foden alizidi kulididimiza jahazi la Juventus dakika ya 69 baada ya kufunga bao lililotokana na mpira wa Mbrazil Savinho ambaye naye alifunga bao la tano kwa shuti kali la nje ya 18
Mshambuliaji wa Kibibi kizee hicho cha Turin Dusan Vlahovic alijipapatua na kuipa Juve goli la pili dakika sita kabla ya mchezo kumalizika lakini isingefua dafu mbele ya mzigo wa mabao Matano ambayo tayari walipokea kutoka kwa vijana wa Pep.
Manchester City watavaana na Al Hilal ya Saudi Arabia katika hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo siku ya Jumanne