Man City yamsajili beki kisiki Gvardiol
MABINGWA wa England Manchester City imekamilisha usajili wa beki kisiki wa kati Josko Gvardiol wa Croatia kutoka RB Leipzig ya Ujerumani kwa pauni milioni 77 sawa na shilingi bilioni 234.85.
Mcroatia huyo ni beki wa pili ghali zaidi kuwahi kusajiliwa England baada ya Harry Maguire aliyejiunga na Manchester United kwa puani milioni 80 mwaka 2019 akitokea Leicester City.
Gvardiol mwenye umri wa miaka 21 amekuwa katika kiwango bora kwa misimu miwili akiwa Leipzig baada ya kujiunga na klabu hiyo Julai 2021 akitokea Dynamo Zagreb.
“Siku zote nimekuwa na ndoto siku moja kucheza England. Kujiunga na City ni kitu maalum sana kwangu na familia yangu,”amesema Gvardiol.
Gvardiol amesema pia atafurahi kucheza timu moja na mshambuliaji mahiri wa City Erling Haaland badala ya kumkaba.
Beki huyo amesema: “Kwa bahati nzuri, niko upande wake sasa na sihitaji tena kumdhibiti.”
“Ni mchezaji tumekuwa tukimfuatilia kwa karibu na tunahisi ana kiwango bora. Vilabu vikubwa kote Ulaya vimekuwa vikimfuatilia, hivyo kumsajili hapa ni habari kubwa kwetu,” amesema Mkurugenzi wa Soka wa City Txiki Begiristain.
Gvardiol alisaidia RB Leipzig kushinda Kombe la Ujerumani katika misimu mwili aliyocheza na pia timu hiyo kufuzu mara mbili Ligi ya Mabingwa Ulaya.