Infantino asifu mashabiki wanawake kujaa uwanjani Iran

ZURICH: Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino amepongeza uamuzi wa shirikisho la soka la Iran kuzipa adhabu ikiwemo kushangiliwa na wanawake tupu klabu za Sepahan SC na Persepolis FC zinazoshiriki ligi kuu nchini humo zitakapokutana mara mbili zijazo.
Uamuzi huo wa shirikisho la soka nchini Iran unakuja baada ya shabiki mmoja wa Sepahan SC kuwashambulia kwa matusi mashabiki wakike wa klabu ya Persepolis FC katika mchezo wa ligi kuu nchini humo uliopigwa katika uwanja wa Azadi stadium mwezi Mei mwaka huu.
Kufuatia adhabu hiyo klabu ya Sepahan SC iliialika Persepolis FC katika uwanja wake wa nyumbani wa Nashq-e Jehan uliopo mjini Isfahan Jumatatu hii ya December 16 mchezo ukihudhuriwa na mashabiki wanawake na wasichana pekee 45,000.
Katika maoni yaliyochapishwa katika mitandao ya kijamii ya FIFA Infantino alisema amefurahishwa sana kuona wanawake na wasichana 45000 waliruhusiwa kuingia uwanjani katika moja ya michezo mikubwa zaidi nchini Iran.
“FIFA imekuwa kwenye mawasiliano ya mara kwa mara na mamlaka za soka za Iran kuhusu masuala ya wanawake na wasichana kuruhusiwa kufurahia mchezo huu pendwa zaidi duniani. Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa kila aliyehusika kufanikisha hili.” taarifa hiyo imemnukuu Infantino.
Ikumbukwe katika kombe la dunia lililopita nchini Qatar mataifa kadhaa yalipaza sauti kwa FIFA kulifungia taifa hilo kushiriki kombe la dunia kutokana na sera zake zisizojumuishi kwa wanawake katika mpira wa miguu ambao FIFA inataka kuufanya mchezo wa watu wote.