Umoja wa Ulaya: Tutaendelea kudhamini na kulinda Utamaduni wa Mzanzibar
ZANZIBAR: NAIBU Balozi Umoja wa Ulaya, Emilio Rossetti amesema sababu kubwa ya wao kuendelea kusaidia maandalizi ya tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar, ZIFF inatokana na wao kupenda kulinda utamaduni wa Mzanzibar kwa sababu ni tunu kwa taifa kwa ujumla.
Balozi huyo amesema hayo katika uzinduzi wa tamasha hilo linaloendelea hadi Agosti 4 visiwani hapa.
Balozi Emilio amesema kingine kinachowavutia kuendelea uwekezaji katika tamasha hilo kwa Tanzania ni kutokana na tamasha hilo kuwa na faida kuwa za moja kwa moja na nyingine zisizo za moja kwa moja akitolea mfano kwamba tamasha hilo ni chanzo cha ajira kwa watu wanaolizunguka kwa kuuza vyakula na wa mahotelini kufanya biashara kwa watalii wanaokuja.
“Tamasha hili linafaida nyingi zilizo za moja kwa moja ikiwemo ajira kwa watendaji wake wasaidizi lakini pia kuna watu wananufaika hata kama siyo moja kwa moja ikiwemo mahoteli makubwa kupata fedha za kigeni kutokana na idadi kubwa ya watalii kuja kutalii visiwani Zanzibar lakini pia kuna wanaonufaika kwa kuuza vyakula, nguo na vitu mbalimbali.” Alisema balozi Emilio
Balozo huyo aliongeza kwa kulihakikishia tamasha hilo kuendelea kupata ufadhili kutoka kwa Umoja wa ulaya kwa kuwa lengo la tamasha hilo linaendana na malengo ya umoja huo kwa mataifa yote wanachama.