LIGI YA MABINGWA AFRIKA>>Yanga, Simba zasaka makundi
MECHI za raundi ya kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zinaanza leo Jumamosi huku wawakilishi wa Tanzania; Simba na Yanga zikianzia ugenini.
Yanga imepangwa kuanza kampeni hizo nchini Rwanda kwa kucheza na Al Merreikh ya Sudan wakati Simba ambayo inaanzia michuano hiyo kwenye raundi hiyo ya kwanza yenyewe itakuwa Ndola, Zambia kucheza na mabingwa wa nchi hiyo, Power Dynamos mechi zote mbili zimepangwa kuanza saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania.
Kuelekea mechi hizo kila upande una matarajio makubwa yakupata ushindi na kutinga hatua inayofuata ya makundi, hiyo ni kutokana na maandalizi ambayo wameyafanya tangu kipindi cha dirisha la usajili hadi sasa ambapo kila timu imeshacheza mechi mbili za ligi na
mechi kadhaa za majaribio.
AL MERREIKH VS YANGA
Yanga ndio mabingwa wa soka wa Ligi Kuu msimu uliopita, wamedhamiria kushinda mchezo huo licha ya kwamba watakuwa ugenini kwenye uwanja wa Pele pale Kigali, Rwanda sababu kubwa ya imani hiyo ni kutokana na ubora wa kikosi chao kilichoimarika mara dufu ukilinganisha na kile kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho na USM Algiers
msimu uliopita.
Yanga inayofundishwa na Kocha Miguel Gamondi raia wa Argentina, imefika hatua hiyo baada ya kuitoa Asas Telecom ya Djibouti kwa matokeo ya jumla ya mabao 7-1 mechi zote mbili zikichezwa uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kuelekea mchezo wa leo, Gamondi anasema ni mchezo mgumu kwa timu zote mbili ingawa anajivunia uzoefu waliokuwa nao asilimia kubwa ya wachezaji wake kwenye michuano hiyo ambayo inasimamiwa na Caf.
“Asilimia kubwa ya wachezaji kwenye kikosi changu wana uzoefu na michuano hiyo ukiwatoa waliokuwepo Yanga msimu uliopita hata baadhi ya wachezaji wageni kama Pacome Zouzoua na Attohola Yao walifika nusu fainali wakiwa na Asec Mimosa kama ilivyo kwa Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ naye alicheza nusu fainali akiwa na Maruma Gallants hivyo sioni kama kuna sababu ya kuwa na hofu,” anasema Gamondi.
Kocha huyo anasema wachezaji ambao hawana uzoefu wa kutosha kwenye michuano hiyo ni Max Nzengeli, Gift Fred na Nickson Kibabage lakini anafurahi kuona wanaenda vizuri na
kukopi kwa haraka kile wanachofanya wenzao.
Kocha huyo anasema amekuwa akiwafuatia wapinzani wao Al Merreikh kuanzia mechi kadhaa za mashindano hayo ikiwemo mchezo wao wa hatua ya awali dhidi ya AS Otoho ya Congo Brazzaville lakini pia mechi za kirafiki ambazo wamecheza hivi karibuni nchini Rwanda.
“Pamoja na ubora tuliokuwa nao lakini nimewaambia wachezaji wangu tucheze kwa tahadhari sababu Al Merreikh ni timu nzuri na wana uzoefu mkubwa kwenye mashindano haya hivyo tunapaswa kucheza kwa umakini mkubwa ili tusipoteze mchezo au kuruhusu
bao,” anasema Gamondi.
Kocha huyo anasema kupitia mchezo huo anataka kuweka rekodi mpya na kuingia kwenye historia ya klabu ya Yanga kwa kuivusha hatua ya makundi baada ya kupita miaka 25 bila timu hiyo kufika hatua hiyo ambapo mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 1998.
Kama alivyosema kocha wa Yanga, Gamondi mchezo hautakuwa rahisi kwani Al Merreikh siyo timu mbaya imekuwa na rekodi za kucheza hatua ya makundi karibu kila msimu ikiwemo msimu uliopita hivyo pamoja na mchezo huo kuchezwa uwanja wa tofauti na nyumbani kwao kwa asili Sudan huenda ukawa mtihani kwa Yanga.
POWER DYNAMOS VS SIMBA
Timu namba saba kwa ubora Afrika, Simba, leo inacheza na mabingwa wa Zambia, Power
Dynamos mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu na wakulipa kisasi kwa wenyeji ambao walifungwa na Simba mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa mwezi uliopita Dar es Salaam.
Ni mchezo mgumu kwa timu zote mbili lakini Simba inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na ubora wa kikosi ilichosajili msimu huu ukilinganisha na wapinzani wao Power Dynamos watakaokuwa nyumbani uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola.
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anasema watatumia ukubwa wao kushinda mchezo huo na kutinga hatua ya makundi kama ilivyozoeleka katika misimu minne iliyopita huko nyuma na hilo litachangiwa na uimara wa kikosi chake.
“Nawaheshimu Power Dynamos ni timu nzuri ina wachezaji vijana wenye uwezo mkubwa lakini Simba ni timu kubwa Afrika na inahofiwa na kujulikana kote duniani hiyo ndiyo silaha
yetu tutacheza soka safi na kupata ushindi mbele ya mashabiki wao,” anasema Robertinho.
Kocha huyo anasema ingawa hawakuanzia hatua ya awali lakini mechi mbili za Ngao ya Jamii na mbili za Ligi Kuu zimemsaidia kuimarisha utimamu wa wachezaji wake na anaamini wapo tayari kuipeperusha Bendera ya Tanzania kufikia malengo yao ambayo ni nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Robertinho anasema usajili walioufanya kwenye dirisha kubwa ni miongoni mwa vitu vinavyompa matumaini ya timu hiyo kufika mbali zaidi kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu wamekamilika tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambapo walikuwa na mapungufu mengi.
“Tuna Willy Esomba Onana, Jose Miquissone, Clotus Chama, Saido Ntibazonkiza na Che Malon hawa wote ni wachezaji wenye chachu kubwa kwenye kikosi chetu, ubora na uzoefu wao naamini utatufikisha mbali kwenye mashindano haya,” anasema Robertinho.