Lewandowski kwenye anga za Ronaldo, Messi
MSHAMBULIAJI wa FC Barcelona Robert Lewandowski ameingia rasmi kwenye kundi la ‘the centurions’ ambalo huwa na wachezaji wenye magoli 100 ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Lewandowski mwenye miaka 36 anaingia kwenye orodha hiyo ambayo ina wababe wawili tu. Cristiano Ronaldo mwenye magoli 140 na Lionel Messi mwenye 129 kupitia bao lake la Penati mnamo dakika ya 10 katika mchezo ambao wababe hao wa La Liga walishinda 3-0 dhidi ya Brest.
Hata hivyo Lewandowski anajiunga na wababe hao akiwa na mashuti 451 ambayo ni machache ukilinganisha na Ronaldo na Messi walipofikisha mabao 100. Ronaldo alifikisha mabao 100 baada ya mashuti 793 na Messi mashuti 527.
Akizungumza na kituo cha TV cha Movistar Plus cha Spain baada ya mchezo huo, Lewandowski amesema ana furaha kufikisha idadi hiyo ya mabao
“nina furaha sana, magoli 101 kwenye ligi ya mabingwa ni namba nzuri sana, sikutarajia ningefikisha magoli mengi hivi kwenye Ligi ya Mabingwa, kujiunga na Messi na Ronaldo natumai wako vizuri” amesema Lewandowski.
Katika mashindano yote msimu huu, Lewandowski sasa amefunga mabao 22 katika mechi 19, mabao tisa zaidi ya mchezaji mwingine yeyote wa La Liga akibakiza mabao manne pekee kuyafikia mabao yake ya msimu uliopita (26 katika michezo 49).